1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schalke na Bremen zakumbwa na shinikizo la mapema

24 Septemba 2020

Schalke na Bremen wako chini ya shinikizo kubwa katika mtanange wao wa wikiendi baada ya kushindwa kupata matokeo mazuri katika siku ya ufunguzi wa mechi za msimu mpya wa ligi kuu ya soka ya Ujerumani, Bundesliga

https://p.dw.com/p/3iwXC
Bundesliga Fussball - Bayern München gegen Schalke 04
Picha: Matthias Balk/dpa/picture-alliance

Matumaini yoyote ya timu za Schalke na Werder Bremen kuzifanya ziweze kusahau msimu mbaya uliomalizika wa ligi kuu ya soka ya Ujerumani, Bundesliga, yalififia katika mechi ya kwanza ya kampeni mpya za kuwania ubingwa wa ligi hiyo, wakati Schalke ilipodhalilishwa kwa kutandikwa mabao 8-0 na mabingwa watetezi Bayern Munich na Bremen nao wakigongwa 4-1 tena wakiwa nyumbani dhidi ya Hertha Berlin.

Sasa timu hizo mbili zinakutana Jumamosi, na shinikizo kubwa kwa kocha mwenyeji David Wagner na mwenzake wa Werder Bremen, Florian Kohfeldt.

Fußball Bundesliga | SV Werder Bremen vs Hertha BSC
Bremen walifungwa 4 - 1 na Hertha BerlinPicha: Martin Rose/Getty Images

Klabu zote mbili ziliendelea kuwa na makocha wake hadi mwisho wa msimu uliopita ambayo Schalke ilimaliza katika nafasi ya 12 baada ya kutopata ushindi katika michezo 16 ya mwisho na Bremen ikimaliza katika nafasi ya 16 tu ikiepuka kushuka daraja kutokana na magoli ya ugenini baada ya kutoka sare mara mbili na timu ya daraja la pili Heidenheim, katika mchezo wa mchujo.

Mkurugenzi wa michezo katika klabu ya Schalke, Jochen Schneider, alisema kuwa hatatamka hadharani tarehe ya mwisho kwa kocha Wagner kuendelea kuionoa timu hiyo, lakini alinukuliwa akisema kuwa kiwango cha ubora kwa timu yake kilichoonyeshwa huko Munich, "hakikubaliki” sasa inahitaji kuboreshwa haraka sana. "Ni wazi kwamba lazima tujionyeshe wenyewe kwa njia tofauti,”alisema Schneider na kuongeza kuwa,”swali muhimu ni kama tunaweza kufanikisha mabadiliko.

Wagner aliongeza kusema kuwa "tutafanikiwa kupanga mambo bara bara. Hiyo inafanya kazi tu na hisia ya mafaniko, kwa sababu hiyo itarejesha ujasiri.”

Bundesliga Fussball - Bayern Munich vs. Schalke 04
Schalke walishushiwa kipigo cha 8 - 0 na Bayern MunichPicha: Matthias Balk/dpa/picture-alliance


Wagner amesisitiza kuwa ana "imani na ubora wa timu yangu kwani sasa wanafanya jaribio jingine kupata ushindi wao wa kwanza tangu Januari.

Schalke wanahitaji sana alama hizo nyumbani kwa sababu michezo yao miwili ya ugenini karibu yote ni migumu ikiwemo ule wa kwanza huko Munich katika mechi dhidi ya RB Leipzig na wapinzani wao wakuu Borussia Dortmund. Wakati huo huo Bremen inatambua ni nini kipo hatarini baada ya kumalizika kwa mchezo wikiendi iliyopita dhidi ya Hertha. Huu ni mkutano wa timu mbili ambazo zilipoteza katika mchezo wa ufunguzi utakuwa mchezo muhimu kwa wiki chache zijazo,”mlinzi wa Bremen Marco Friedl alisema.”Kila mmoja wetu anajua kilicho hatarini katika mchezo dhidi ya Schalke.

Kohfeldt alikiri kiwango cha ubora kwa timu yake dhidi ya Hertha hakikuwa kizuri kwa michuano hiyo ya Bundesliga kwa njia nyingi na meneja mkuu Frank Baumann amehimiza timu hiyo kugundua tena imani hiyo katika mchezo wao.

Deutschland Bundesliga | Fortuna Duesseldorf vs FC Schalke 04 | Trainer David Wagner
Chuma cha kocha Wagner kipo motoniPicha: picture-alliance/dpa/M. Meissner

Klabu zote mbili hazina nafasi ya kuongeza wachezaji katika dirisha la usajili ambalo limebaki wazi hadi Oktoba 5 kwa sababu ya ukata wa pesa baada ya mapato kupungua kufuatia mlipuko wa janga la virusi vya Corona.

Mwiba wa hivi karibuni katika visa vya Covid 19 katika mkoa huo, pia umefanya kuwepo na sintofahamu ya mashabiki kuhudhuria mchezo huo. Schalke inatarajia kuwa na mashabiki 11,000 lakini hawataanza kuuza tiketi hadi siku ya Ijumaa.

Pia siku ya Jumamosi Bayer Leverkusen watawakaribisha Leipzig katika mechi inayozikutanisha timu mbili ambazo zimepoteza nyota wao bora waliosajiliwa na klabu ya Chelsea Kai Havertz and Timo Werner.

Pilika pilika za ligi kuu ya Bundesliga wekiendi hii zinaanza Ijumaa na mchezo kati ya Hertha dhidi ya Eintracht Frankfurt. Na Jumamosi michezo mingine ni Borussia Moenchengladbach dhidi ya Union Berlin, Mainz watakipiga na VfB Stuttgart, Augsburg dhidi ya Borussia Dortmund na Arminia Bielefeld dhidi ya Cologne. Ratiba ya Jumapili ni Hoffenheim dhidi ya Bayern na Freiburg dhidi ya Wolfsburg.

Mwandishi: Deo Kaji Makomba/dpa

Mhariri: Bruce Amani