Schalke wakamata nne, Düsseldorf watimuliwa
20 Mei 2013Hata hivyo waliotabasamu zaidi walikuwa ni vijana wa Schalke 04. Schalke wametia mfukoni tikiti ya kucheza Champions League msimu ujao baada ya kusajili ushindi wa magoli mawili kwa moja nyumbani kwa Freiburg. Schalke wamemaliza msimu katika nafasi ya nne na watacheza mchuano wa mikondo miwili ya kufuzu katika Champions League katika msimu ujao. Freiburg nao wamemaliza katika nafasi ya tano na watacheza katika Europa League.
Eintracht Frankfurt pia watajiunga na Freiburg katika dimba la Europa League, baada ya kumaliza katika nafasi ya sita kufuatia sare ya magoli mawili kwa mawili na Wolfsburg. Hayo ni mafanikio makubwa sana kwa klabu ya Frankfurt ambayo ilipandishwa daraja tena kurudi katika Bundesliga mwaka wa 2012.
VfB Stuttgart ambao walitoka sare ya mabao mawili kwa mawili na Mainz, wamefuzu moja kwa moja katika Europa League, kwa sababu walifuzu katika fainali ya kombe la Shirikisho la Ujerumani – DFB Pokal dhidi ya Bayern Munich, itakayochezwa Juni mosi. SV Hamburg walimaliza wa saba kwenye msimamo wa ligi, na kukosa fursa ya kucheza Ulaya, baada ya kuduwazwa goli moja kwa sifuri nyumbani na Bayer Leverkusen. Stefan Kiessling aliifungia Leverkusen goli hilo la pekee, na kufanya idadi ya mabao aliyotia kimyani msimu huu kufika 25. Bidii hiyo ilimpa tuzo ya kuwa mfungaji bora wa Bundesliga msimu huu.
Kiessling mfungaji bora
Kiessling alimpiku nyota wa Borussia Dortmund Robert Lewandowski ambaye alifunga mabao 24. Augsburg, ambao walikuwa katika kundi la timu tatu zilizoshika mkia kwa kipindi kirefu cha msimu, walisababisha mshangao mkubwa kwa kuwashinda mabao matatu kwa moja Greuther Fürth ambao tayari waliiaga Bundeliga. Hoffenheim walimaliza katika nafasi ya 16 nafasi moja nyuma ya Augsburg, baada ya ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya nambari mbili Borussia Dortmund. Ushindi huo una maana kuwa Hoffenheim watacheza mechi ya mchujo dhidi ya timu ya tatu bora kutoka Ligi ya daraja ya tatu, Kaiserslauten.
Waliokuwa na kilio kikubwa katika siku hii ni Fortnuna Düsseldorf. Walikuwa katika nafasi ya 15 kabla ya mechi za siku ya mwisho kung'oa nanga, wakapata kipigo cha mabao matatu kwa sifuri nyumbani kwa Hanover na wakamaliza ligi wakiwa katika nafasi ya pili kutoka nyuma. Sasa wameteremka moja kwa moja hadi daraja ya pili. Mechi ya mwisho ya Bundesliga ya Jupp Heynckes akiwa kocha wa Bayern Munich ilimpeleka nyumbani Borussia Mönchengladbach, klabu ambayo alianzia taaluma yake ya kabumbu na ukufunzi. Licha ya mechi hiyo kuwa na sarakasi nyingi, Bayern hatimaye walipata ushindi wa mabao manne kwa matatu huku Frank Ribery akionesha usogora wa hali ya juu.
Jupp Heynckes aiaga Bundesliga
Bayern sasa wamemaliza msimu wakiwa na rekodi chungu nzima, ikiwa ni pamoja na kukusanya jumla ya pointi nyingi sana kuwahi kushuhudiwa, 91. Wamerarua kurasa za madaftari ya kumbukumbu kama timu bora kabisa ya Bundesliga, na wana fursa ya kuweka historia ya kushinda mataji matatu msimu huu. Werder Bremen ilipoteza mchuano wake wa kwanza baada ya kuondoka kocha wao wa muda mrefu Thomas Schaaf kwa kushindwa mabao matatu kwa mawili na Nuremberg.
Humels anaelekea kupona
Tuangazie kidogo sasa ligi ya mabingwa Ulaya, ambapo huku zikiwa zimesalia siku nne tu kwa fainali kubwa inayosubiriwa na ulimwengu mzima, uwanjani Wembley jijini London, beki wa Borussia Dortmund, Mats Hummels anatarajiwa kupona jeraha la kifundo cha mguu kabla ya fainali hiyo dhidi ya Bayern Munich. Hummels, alijeruhiwa Jumamosi katika mchuano wa Bundesliga, lakini daktari wa timu amesema Hummels bila shaka ataweza kucheza katika uwanja wa Wembley. Mshambuliaji Mario Götze anarejea katika mazoezi ya kikosi kesho na atakuwa tayari kwa fainali hiyo kubwa ya Champions League. Huo utakuwa mchuano wake wa mwisho katika timu ya Dortmund kabla ya kuhamia Bayern.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman