1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schalke yaiteka Galatasaray mjini Istanbul

21 Februari 2013

Schalke imeendeleza matokeo yake bora ya kutoshindwa katika Ligi ya Mabingwa, baada ya kulazimisha sare ya goli moja kwa moja dhidi ya Galatasaray. Nao Barcelona waliduwazwa na AC Milan 2 - 0, uwanjani San Siro

https://p.dw.com/p/17iWP
Schalke 04's Jermaine Jones (R) celebrates his goal against Galatasaray during their Champions League soccer match at Turk Telekom Arena in Istanbul February 20, 2013. REUTERS/Murad Sezer (TURKEY - Tags: SPORT SOCCER)
Fußball Champions League Schalke 04 Galatasaray IstanbulPicha: Reuters

Lakini mfungaji wa goli la Schalke, kiungo Jermaine Jones atakosa mchuano wa mkondo wa pili wa awamu ya mchujo mnamo tarehe 12 Machi, baada ya kukusanya kadi yake ya tatu ya njano katika dimba hilo, dakika kumi kabla ya kutikisa wavu.

Mshambuliaji Mturuki Burak Yilmaz alifungua ukurasa wa magoli kwa kufunga goli maridadi na lenye ufundi wa hali ya juu, baada ya kuudhibiti mpira kwa kisigino kabla ya kusukuma kombora kali lililomzidi nguvu kipa wa Schalke Timo Hildebrand. Licha ya kuwa macho yote yalikuwa yanaangaziwa mshambuliaji Didier Drogba na Wesley Scheider, Yilmaz ndiye aliyewafurahisha mashabiki kwa kufunga goli lake la saba katika mechi saba za Champions League.

Schalke wana faida ya goli la ugenini kabla ya mchuano wa mkondo wa pili nyumbani Ujerumani
Schalke wana faida ya goli la ugenini kabla ya mchuano wa mkondo wa pili, nyumbani UjerumaniPicha: Reuters

Lakini Schalke walijibu muda mfupi kabla ya kipindi cha kwanza kukamilika, baada ya Jefferson Farfarn kumwandalia pasi Klaas Jan-Huntelaar ambaye hakuchelewa kumpakulia Jermaine Jones aliyesukuma mkwaju maridadi wavuni.

Barca waachwa midomo wazi

Katika mchuano mwingine wa kuvutia, Matumaini ya Barcelona ya kushinda kombe la Ligi ya Mabingwa kwa mara ya nne katika misimu minane yananing'inia hewani baada ya kuduwazwa na AC Milan kwa magoli mawili bila jawabu. Barca huenda wamelishika kwa mkono mmoja taji la Ligi ya Uhispania La liga, lakini walizidiwa maarifa na Milan katika uwanja ambao pia walinyamazishwa na Inter Milan katika nusu fainali za mwaka wa 2010.

Jinsi iloivyo desturi yao, Barca walitawala ndani ya uwanja wa San Siro kwa kuumiliki mpira lakini wakalazimika kulipia ukosefu wa mbinu na maarifa kwa sababu walilijaribu lango la Milan mara mbili pekee usiku mzima..

Magoli ya kipindi cha pili kutoka kwa wachezaji wawili wa Ghana Kevin Prince Boateng na Sulley Muntari yaliiwacha Barca na kibarua kigumu katika mkondo w apili baada ya usiku ambao Lionel Messi alinyamazishwa kabisa uwanjani na hakufanya mambo yake tunayomfahamu kufanya….Barcelona walikasirishwa na goli la kwanza wakati mpira ulipoonekana kuugonga mkono wa Cristian Zapata kabla ya kuanguka mbele ya Boateng ambaye alisukuma kombora langoni.

Barcelona walikuwa an usiku mrefu katika uwanja wa San Siro, na wana kibarua nyumbani Camp Nou
Barcelona walikuwa an usiku mrefu katika uwanja wa San Siro, na wana kibarua nyumbani Camp NouPicha: Getty Images

kocha msaidizi wa Barca Jordi Roura amesema matokeo yako jinsi yalivyo, licha ya kuwa waliudhibiti mchezo, ijapokuwa hawakutengeneza nafasi nyingi za kufunga jinsi tu walivyokosa pia Milan. Roura amesema matokeo hayo hayafurahishi lakini wana matumaini ya kuyageuza katika mkondo wa marudiano kwa usaidizi wa mashabiki wao wa nyumbani.

Naye kocha wa Milan Massimiliano Allegri alikuwa mwepesi kusema vijana wake walistahili ushindi huo. Amesema walicheza vyema katika safu ya ulinzi, na kwamba mchezo huu bado uko wazi hadi dakika ya mwisho.

Mechi za Europa League

Hii leo itakuwa zamu ya timu zinazocheza katika daraja la pili la kinyang'anyiro cha Ulaya, Europa League, ambapo timu nne za Bundesliga ya hapa Ujerumani zitakuwa miongoni mwa mechi za mkondo wa marudiano wa awamu ya timu 32 za mwisho. VfB Stuttgart wako mjini Ubelgiji kupambana na Genk wakati Borussia Moenchengladbach wakiangushana na Lazio mjini Rome Italia. Hanover watakuwa wenyeji wa Anzi Makhachkala wa Urusi wakati Bayer Leverkusen wakipambana ugenini na Benfica nchini Ureno.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters

Mhariri: Sekione Kitojo