Schalke yamfutakazi kocha wake Wagner
27 Septemba 2020Schalke 04 inayotambulika kama majogoo wa bluu ya Kifalme wamekandamizwa mabao 11 na kufunga bao moja tu katika michezo yake miwili ya mwanzo wa msimu huu. Kipigo cha mabao 3-1 siku ya Jumamosi nyumbani dhidi ya Werder Bremen kimekuja baada ya kipigo cha mbwa mwizi cha mabao 8-0 katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya mabingwa wa ligi Bayern Munich.
"Tulitarajia kwamba tungeweza kufanya mabadiliko ya kimchezo yanayohitajika kwa pamoja na david Wagner," Mkuu wa spoti na mawasiliano Jochen Schneider alinukuliwa akisema katika taarifa ya klabu hiyo. "Kwa bahati mbaya michezo yetu miwili ya mwanzo ya msimu mpya hayakuleta mchezo unaohitajika na matokeo."
Makocha wasaidizi wa Wagner , Christoph Buehler na Frank Froehling pia wamevuliwa madraka yao. Mrithi wa kazi ya Wagner mwenye umri wa miaka 48 bado hajatangazwa. Wanaofikiriwa kuchukua nafasi hiyo ni pamoja na kocha wa zamani wa Mainz Sandro Schwarz , kocha wa zamani wa Augsburg Manuel Baum, kocha wa zamani wa Stuttgart Alexander Zorniger na Marc Wilmots, kocha wa zamani wa Ubelgiji ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Schalke.
Kocha wa nne kutimuliwa baada ya michezo miwili
Katika misimu 58 ya Bundesliga, Wagner ni kocha wa nne kuondolewa katika wadhifa wake baada ya michezo miwili. Wengine ni Rinus Michels (FC Cologne, 1983)Morten Olsen(FC Cologne, 1995) na Dieter Hecking (Hanover,2009).
Wagner, ambaye alicheza kandanda akiwa na Schalke katikati ya miaka ya 1990, alifungishwa mkataba hadi mwaka 2022.
Wagner aliteuliwa kuipa mafunzo Schalke 04 majira ya joto mwaka jana na aliisaidia Schalke kufikia nafasi ya tano katika msimamo wa ligi katikati ya Januari baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Borussia Moenchengladbach kuwafikisha pointi tatu tu nyuma ya waliokuwa hatimaye mabingwa Bayern Munich.
Lakini Schalke haijashinda mchezo wa ligi tangu wakati huo , na Wagner amepoteza kazi yake kutokana na hali hiyo ya kushindwa.