Schalke yazinduka katika Bundesliga
3 Oktoba 2016Manchester City yaonja kipigo chini ya Pep Guardiola , na majirani zao Manchester United yaambulia sare mbele ya Tottenham Hotspurs.
Katika Bundesliga, Schalke 04 ilifikisha mwisho masaibu yake ya kupokea vipigo mfululizo msimu huu ambapo timu hiyo ilikubali vipigo mara tano katika msimu huu wa ligi na kujinasua kutoka mkiani mwa ligi jana Jumapili kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Borussia Moenchengladbach wakati mchezaji aliyesainiwa hivi karibuni Breel Embolo akifumania nyavu mara mbili.
Embolo mwenye umri wa miaka 19 , na kuigharimu Schalke kitita cha euro milioni 22 kutoka Basel ya Uswisi mwezi Juni , alifunga mabao yake ya kwanza kwa Schalke katika kipindi cha pili baada ya kuwa sare bila kufungana katika kipindi cha kwanza.
"Nimefurahi kufunga mabao, lakini kitu muhimu ni kwamba tumeshinda na tumenufaika na mchezo mzuri tuliouonesha", amesema Embolo.
Mshambuliaji wa Borussia Moenchengladbach Andre Hahn hakufurahishwa na timu yake ilivyocheza.
"Kwa ufupi hatukufanya vizuri. Katika kipindi cha kwanza hatukuweza kucheza vizuri na katika kipindi cha pili tulijaribu kubadilika, lakini ndipo Schalke ikapata penalti. Na kuanzia hapo wapinzani wetu waliongeza ari na tulizidi kuharibikiwa, ulinzi mbovu na kisha tukaendelea kufungwa mabao.
Matokeo hayo yameinyanyua Schalke hadi nafasi ya 16 katika timu 18 za ligi ya Bundesliga, na kuicha Hamburg ikiwa mkiani mwa ligi hiyo baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Hertha Berlin ikiwa ni kipigo cha tano mfululizo. Gladbach ambayo ilipoteza mchezo wake dhidi ya Barcelona siku ya Jumatano katika Champions League , imeporomoka hadi nafasi ya 9 katika msimamo wa ligi.
Katika mchezo wa kwanza jana Jumapili ukame wa magoli kwa mshambuliaji mpya wa Wolfsburg Mario Gomez uliendelea baada ya kutoka sare bila kufungana na Mainz 05.
Huyu hapa Mario Gomez.
"Sio tu mashabiki wamevunjika moyo, lakini hata sisi. Leo tulifanya juhudi kupita kiasi. Nitasema nini ? Ni balaa, kwa kweli ni balaa, mpira ulikuwa hautaki kabisa kuvuka msitari. Hatujajizawadia kwa mchezo wetu , kwa kweli tulikuwa na nafasi nyingi , na tungeweza kushinda mchezo huo kwa mabao mengi.
Lakini Gomez hadi sasa ameshindwa kuutumbukiza mpira wavuni kwa dakika 450 katika Bundesliga na kuwa na jioni ya kufadhaisha katika uwanja wa Volkswagen Arena jana. Wolfsburg imepata ushindi mara moja tu katika michezo sita ya ligi msimu huu. Sare hiyo imeiweka Wolfsburg , ambayo ilifikia robo fainali ya Champions League msimu uliopita , ikiwa nafasi ya 13 ya msimamo wa ligi ya Ujerumani na Mainz ikiwa katika nafasi ya 11.
Lakini timu inayoshangaza msimu huu ni FC Kolon ambayo haijaonja kipigo hadi sasa katika Bundesliga , na mwishoni mwa juma ilitoroka na pointi moja mbele ya mabingwa watetezi Bayern Munich katika uwanja wa Alianz Arena mjini Munich baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.
Huyu hapa kocha wa FC Kolon Peter Stoeger.
"Iwapo utaweza kupata pointi mjini Munich , basi unafarijika sana. Tunatambua, kwamba mchezo huo haukuwa rahisi. Ni wazi , kwamba katika dakika 45 za kwanza hawakuweza kufanya mengi, kuliko tulivyofanya. Kipindi cha pili kilikuwa kizuri , kwa hiyo kwetu hali ilikuwa nzuri. Tunafurahi jinsi tulivyofanyakazi kwa pamoja , ni mara ya kwanza kwetu kupata pointi dhidi ya bayern. Na inafurahisha.
Mshambuliaji wa Bayern Munich Thomas Mueller alikuwa na haya ya kusema baada ya mchezo huo.
"Hatukucheza vizuri kuanzia kipindi cha pili kilipoanza hadi dakika ya 70. Kuanzia hapo mara kadhaa tuliyumba, na dakika za mwisho tulipata bahati, kwa kuwa tulijiingiza katika hatari. Tulitaka kulinda ushindi wetu kwa kila hali. Katika kipindi cha pili tulikosa bahati katika kumalizia mipira golini. Kwa jumla ni kawaida kwamba haikuwa mbaya sana , wakati unaongoza kwa bao 1-0 nyumbani na hatimaye unaambulia tu pointi moja."
Borussia Dortmund haikuweza kuhimili vishindo vya Bayer Leverkusen baada ya kutoka sare ya Real Madrid katikati ya wiki , na kukubali kipigo cha mabao 2-0 katika uwanja wa Bayer Arena mjini Leverkusen. Mbali ya kubadilisha benchi la ufundi na kuamua kumpa jukumu hilo kocha Markus Gisdol baada ya kumfuta kazi Bruno Labbadia hamburg SV ilijikuta ikigaagaa mchangani tena baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Hertha Berlin. Huyu hapa kocha Markus Gisdol.
"Unaweza kuona kwamba ni siku chache tu tumekuwa pamoja. Na kumekuwa na matukio mazuri yaliyoonekana uwanjani. Ni kweli kwamba kuna mambo mengi, ambayo tunapaswa kuyafanya vizuri zaidi. Lakini ishara ya kwanza , ambayo timu imeionesha , naona sio mbaya. Kwa bahati kidogo tu huenda leo tungeweza pengine kupata kitu.
Premier League yawaka moto
Nchini Uingereza , katika premier league wiki hii pia kumetokea mengi , ambapo timu mbili ambazo hazijapoteza mchezo Tottenham Hotspurs na Manchester City zilikutana na kulitarajiwa kutokea kitu jana Jumapili. Kikosi cha kocha Mauricio Pochettino kilikizawadia kikosi cha Pep Guardiola kipigo cha kwanza msimu huu kwa ushindi wa bao 2-0.
Ushindi huo umeondoa mtazamo kutoka kampeni ya City katika msimu huu kuanza kwa kasi ya ajabu hadi katika kile ambacho kimekuwa mwanzo mzuri kabisa wa Spurs tangu msimu wa mwaka 1960-61 wakati timu hiyo iliposhinda ligi na kombe la FA.
Kwingineko pia kulikuwa na sare ambapo Stoke City ilitoka sare ya bao 1-1 na Manchester United na Southampton ikalazimisha sare ya bila kufungana na mabingwa watetezi Leicester City.
Na katika uwanja wa Turf Moor kocha wa Arsenal Arsene Wenger alikuwa akisherehekea miaka 20 akiwa kocha wa The Gunners na kushuhudia timu yake ikinyakua ushindi katika dakika ya mwisho wakati wenyeji wakidhania kwamba wamepata sare. Arsenal iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Burnley.
Wakati huo huo Swansea City imemfuta kazi kocha wake Francesco Guidolin na kumwajiri haraka kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Marekani Bob Bradley kuchukua nafasi yake.
Ligi ya Uhispania nguvu ya tatu yatawala
Atletico Madrid inaongoza ligi ya Uhispania , La Liga baada ya kuishinda Valencia jana Jumapili kwa mabao 2-0, ambapo siku hiyo ilishuhudia mabingwa Barcelona ikipokea kipigo cha mabao 4-3 dhidi ya Celta Vigo na Real Madrid ikitolewa jasho na Eibar kwa kutoka sare ya bao 1-1.
Bao safi la Mario Balotelli dakika nne kabla mpira kumalizika uliipa Nice ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Lorient jana na kuiweka timu hiyo ya Ligue 1 juu ya msimamo wa ligi kwa kipindi hiki ligi za Ulaya zinaposita kwa ajili ya michezo ya timu za taifa.
Katika Serie A ligi ya Italia Udinese imemfuta kazio kocha wake Giuseppe Iachini baada ya kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Lazio kipigo cha nne mfululizo katika michezo saba ya ligi.
Ubingwa wa Nigeria
Barani Afrika Rangers ya Nigeria jana walitawazwa mabingwa wa ligi ya soka ya nchi hiyo baada ya kusubiri kwa miaka 32 wakati walipoitwanga El Kanemi Warriors kwa mabao 4-0 na kumaliza wakiwa juu ya msimamo wa ligi katika siku ya mwisho ya ligi ya nchi hiyo. Rangers wamemaliza wakiwa na pointi 63 kutokana na michezo 36, pointi tatu juu ya washindi wa pili Rivers United. Timu hizo sasa zitaiwakilisha nchi hiyo katika champions League barani Afrika.
Mchezaji wa zamani wa Liverpool Rigobert Song, nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon , mwenye umri wa miaka 40, amekuwa katika hali ya kutojitambui leo Jumatatu akiugua kiharusi. Radio ya taifa ya Cameroon imerikopti kuwa Song, ambae pia aliichezea West Ham United, Metz na Lens za Ufaransa, FC Kolon ya Ujerumani na Galatasaray ya Uturuki, alikimbizwa hospitali ya karibu na Yaounde jana Jumapili baada ya kupata uvimbe katika ubongo.
Marais wa shirikisho la kandanda barani Afrika CAF watawekewa ukomo wa vipindi vitatu vya miaka minne kuanzia uchaguzi utakaofanyika mwaka 2017, taasisi hiyo inayosimamia michezo barani Afrika imesema leo. Hakujakuwa na ukomo hapo kabla ambapo rais wa sasa Issa Hayatou aliliongoza shirikisho hilo la Afrika tangu mwaka 1988.
Na katika mchezo wa golf
Marekani iliwashinda wachezaji wa bara la Ulaya kwa 17-11 katika ubingwa wa Ryder Cup katika mchezo wa golf ukiwa ni ushindi wa kwanza tangu mwaka 2008, kombe ambalo hushindaniwa baina ya wachezaji wa golf wa Ulaya na Marekani kila mwaka .
Nae Sebastian Vettel wa mbio za magari za Formula 1 ameomba radhi kwa kugongana na Nico Rosberg mwanzoni mwa mbio za magari za Malaysia Grand Prix, alipompigia simu Rosberg jana Jumapili. Dereva huyo wa gari aina ya Ferrari alimgonga Rosberg katika kona akijaribu kumpita, lakini aliishia kuharibu gari yake na kumlazimisha Rosberg kupunguza kasi na kurudi nyuma, hata hivyo Rosberg alimaliza akiwa namba tatu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe / rtre / dpae
Mhariri : Yusuf , Saumu