Scholz aahidi mshikamano na Italia juu ya sera ya hifadhi
8 Juni 2023Kansela Scholz, alipozungumza mjini Berlin kabla ya kuanza ziara yake amesema Italia, Ugiriki na nchi nyingine za kusini mwa Ulaya zinakumbwa na changamoto ya idadi ya wakimbizi inayozidi kuongezeka. Amesema Ujerumani haipaswi kuziacha nchi hizo peke yao, akipendekeza badala yake mshikamano na uwajibikaji kutoka nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Hiyo ni ziara yake ya kwanza Italia tangu Meloni, mwanasiasa wa sera kali za mrengo wa kulia alipoingia madarakani Oktoba mwaka jana. Waziri Mkuu Meloni pia alifanya ziara mjini Berlin mwezi Aprili, na wakati huo Kansela Scholz alibainisha nia ya kuendeleza ushirikiano wa karibu na kiongozi huyo mpya, na kuongeza kuwa makubaliano na serikali ya awali yangeendelea kuzingatiwa bila mabadiliko.