1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz asema hatoipa Ukraine makombora ya Taurus

21 Septemba 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesisitiza msimamo wa kutoipa Ukraine makombora ya masafa marefu katika jaribio lake la kuwashawishi wapiga kura katika jimbo la Brandenburg.

https://p.dw.com/p/4kvBZ
Sommerreise von Bundeskanzler Scholz
Kansela Olaf Scholz akizungumza na wakaazi wa Brandenburg wakati wa ziara yake katika jimbo hilo la mashariki mwa Ujerumani.Picha: Thomas Koehler/photothek/IMAGO

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amekuwa akifanya kampeni kwa ajili ya chama chake cha Social Democratic SDP kabla ya uchaguzi wa siku ya Jumapili katika jimbo la Brandenburg, mashariki mwa Ujerumani ambako chama chake kinapambana na chama cha mrengo mkali wa kulia Alternative für Deutschland AfD.

Kiongozi huyo amewahakikishia wapiga kura kwamba Ujerumani haitoipa Ukraine makombora aina ya Taurus, licha ya Kyiv kuwahimiza washirika wake wa Magharibi kuipa silaha zaidi ili kukabiliana na wanajeshi wa Urusi katika uwanja wa vita.

"Ingawa wengi wamejaribu kunirai, sitatoa makombora ya masafa marefu ambayo yana uwezo wa kufika hadi Moscow," Scholz ameuambia mkutano uliofanyika Brandenburg.

"Nawahakikishia hili: Nitashikilia msimamo huu."

Soma pia:  Scholz na upinzani wabumburushana bungeni kuhusu uhamiaji

Jimbo la Brandenburg linaongozwa na Dietmar Woidke wa chama cha SPD, japo chama hicho kinakabiliwa na upinzani na AfD kuelekea uchaguzi wa siku ya Jumapili.

Ukraine imekuwa ikipambana na wanajeshi wa Urusi kwa zaidi ya miaka miwili na nusu. Licha ya kuungwa mkono na mataifa ya Magharibi, vita hivyo vimeenea hadi ndani ya Urusi baada ya vikosi vya Ukraine kuliteka eneo la Kursk katika hatua ambayo huenda ikamshurutisha Rais Vladimir Putin kwenye meza ya mazungumo.

Scholz anatumai kuwa chama cha SPD kitashinda uchaguzi huo, akitaja ukuaji wa uchumi ulioshuhudiwa jimboni humo katika miaka ya hivi karibuni kama moja ya sababu ya kukiamini chama hicho.

“Kwangu mimi, ni muhimu sana kwa Brandenburg kuendelea kupiga hatua za maendeleo katika siku zijazo,“ Kansela huyo ameliambia shirika la habari la dpa katika ziara ya awali aliyoifanya katika maonyesho ya filamu katika mji mkuu wa jimbo hilo, Potsdam karibu na Berlin.