Scholz kwenda Moldova na kujadili athari za vita vya Ukraine
21 Agosti 2024Matangazo
Scholz atafanya mazungumzo na Rais wa Moldova Maia Sandu na Waziri Mkuu Dorin Recean katika mji mkuu wa nchi hiyo. Mazungumzo yake yatajikita katika athari za vita vya Urusi nchini Ukraine kwa nchi hiyo ndogo na wakaazi wake milioni 2.6. Serikali ya Moldova ambayo inatafuta kuwa mwanachama wa Umojawa Ulaya inaituhumu Urusi kwa kutoa taarifa za uongo kwa kukusudia na kuiyumbisha nchi hiyo. Urusi ina kituo cha majeshi yake katika eneo lililojitenga la Transnistria tangu miaka ya tisini. Scholz aliizuru Moldova mwaka jana kwa ajili ya mkutano wa kilele wa Ulaya ila ziara yake ya sasa ndiyo ya kwanza ya baina ya nchi na nchi kufanywa na Kansela wa Ujerumani katika kipindi cha miaka 12.