Scholz na Macron waadhimisha miaka 60 ya mkataba wa Elysee
22 Januari 2023Wamesema hayo kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 60 tangu kutiwa saini mkataba wa urafiki kati ya nchi hizo mbili.
Hata hivyo kuna mikwaruzano inayohusu kurekebisha ushirikiano na uongozi wao ndani ya Umoja wa Ulaya. Mkataba wa nchi mbili hizo ni hati iliyofanikisha kuwekwa mkakati wa ushirikiano katika sera za kigeni, ulinzi na utamaduni.
Msemaji wa Elysee amewaambia waandishi wa habari kwamba maadhimisho hayo hiyo yanadhihirisha jinsi uhusiano wa Ufaransa na Ujerumaniulivyo na kwamba nchi hizo zinasonga mbele kwa pamoja barani Ulaya.
Mada kuu zilizojadiliwa kwenye mkutano ni ushirikiano katika sekta ya ulinzi, sera ya viwanda, nishati, mageuzi katika Umoja wa Ulaya na uhamiaji. Wachambuzi wanasema umma utayafuatilia kwa karibu iwapo viongozi hao Emmanuel Macron na kansela wa Ujerumani Olaf Scholz watafanikisha malengo hayo.
Chanzo cha mvutano kati ya Ujerumani na Ufaransa:
Mkutano wa kila mwaka wa Baraza la Mawaziri wa nchi mbili hizo, uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka uliopita, ulivunjwa. Mabadiliko hayo ya ratiba yalionesha kilele cha mivutano iliyodumu kwa miezi kadhaa na ugumu uliozidi katika uhusiano kati ya nchi mbili hizo.
Wakati huo, Ujerumani, pamoja na mambo mengine, ilitia saini mkataba wa mfumo mpya wa ulinzi wa anga wa Ulaya ambao haukuijumuisha Ufaransa jambo lililoifanya Ufaransa kuanzisha kivyake mpango kama huo kati yake na Italia. Ufaransa nayo ilifikia makubaliano juu ya ujenzi wa bomba jipya la hidrojeni na gesi na Uhispania na Ureno, ikipuuzilia mbali mradi unaopendelewa na Ujerumani. Rais Macron pia aliilaumu Ujerumani hadharani kwa kujitenga.
Hata hivyo kulingana na Stefan Seidendorf, naibu mkurugenzi wa taasisi ya wataalamu ya Ludwigsburg inayoshughulikia maswala ya Ujerumani na Ufaransa - (DFI), mkutano huo wa mawaziri ambao haukufanyika ulikuwa kama mbiu ya kuziamsha pande hizo mbili.
Seidendorf ameiambia DW kwamba maafisa wa serikali ya Ujerumani walishangazwa na shinikizo kutoka kwa umma juu ya mivutano hiyo. Amesema maafisa hao walidhani kwamba uhusiano kati ya Ufaransa na Ujerumani ungeendelea tu bila kujitokeza matatizo yoyote lakini haikuwa hivyo. Hata hivyo uhusiano wa Ujerumani na Ufaransa wakati wote umo katika muundo wa mwafaka.
Vita vya Ukraine:
Juu ya vita vya nchini Ukraine, Ujerumani na Ufaransa zimeahidi kuendelea kusimama pamoja na nchi hiyo kwa kadri itakavyowezekana.
Mkataba kati ya Ujerumani na Ufaransa ulitiowa saini mnamo mwaka 1963 uliweka msingi wa ushirikiano baina ya mataifa hayo ambayo hapo awali yalikuwa hasimu.
Vyanzo: AP/AFP/DW