1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schulz aukubali mwaliko wa Rais Steinmeier

24 Novemba 2017

Kiongozi wa chama cha Social Democrats nchini Ujerumani Martin Schulz ameubadili msimamo wake na kusema kwamba chama chake kitashiriki mazungumzo ya kuunda serikali mpya.

https://p.dw.com/p/2oDCX
Berlin Martin Schulz, SPD-Parteivorsitzender
Kiongozi wa chama cha SPD cha Ujerumani Martin SchulzPicha: picture-alliance/dpa/M. Gambarini

Hatua hii inaleta matumaini ya kuukwamua mkwamo wa kisiasa uliokuwapo tangu kukamilika kwa uchaguzi wa kitaifa mwezi Septemba.

Martin Schulz aliwaambia waandishi habari mjini Berlin kwamba chama chake sasa kiko tayari kukutana na vyama vyengine lakini akasisitiza kwamba mazungumzo hayo hayatochukua tu mwelekeo mmoja.

Tamko hili la Schulz linakuja baada ya Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier kutoa mwaliko kwa vyama vyote husika na wakuu wake akiwemo Kansela Angela Merkel, Mkuu wa chama cha CSU, Horst Seehofer, na Schulz, wakutane wiki ijayo kwa mazungumzo yatakayojikita katika kuundwa kwa serikali mpya.

Schulz amebadili msimamo kuhusiana na mazungumzo

"Tumekubaliana kwamba bila shaka niukubali mwaliko wa Rais wa Ujerumani wa kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vyengine. Na bila shaka SPD itaendelea kufanya kazi katika serikali ya mpito," alisema Schulz. "Kutakuwa na mazungumzo mengi katika siku na wiki zijazo. Tutafanya mazungumzo ya kina kwa kila hatua tutakayopiga, katika ngazi ya chama na uongozi."

Rais wa Ujerumani Steinmeier
Rais wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: picture-alliance/abaca/M. Gambarini

Hatu hii inaonesha kubadili msimamo kwa Schulz ambaye alikuwa ameuondoa uwezekano wa kushiriki mazungumzo yoyote ya kuunda serikali ya mseto baada ya kushindwa na Kansela Merkel katika uchaguzi wa Septemba 24. Alisema chama hicho kimeamua kubadili msimamo baada ya mkutano wake na Steinmeier hapo jana.

Steinmeier alivitaka vyama vyote vikutane kwa mazungumzo baada ya Merkel kushindwa kuunda serikali katika mazungumzo aliyoyafanya na chama cha Kijani na kile cha Free Democrats. 

Schulz lakini alisema kwamba wao kama viongozi wa SPD hawatojiamulia suala lolote bali iwapo kutakuwa na suala la maamuzi basi watalipeleka mbele ya wanachama wao na lipigiwe kura, jambo ambalo huenda likachelewesha zaidi kuundwa kwa serikali mpya.

Merkel amekuwa tayari kwa mazungumzo

"Hakuna kitu chochote ambacho ni cha moja kwa moja katika njia tunayoelekea. Lakini kitu kimoja kiko wazi kabisa," alisema Schulz, "iwapo majadiliano yatafikia katika suala la sisi kuamua kushiriki kwa njia yoyote ile katika kuundwa kwa serikali, tutaliwasilisha mbele ya wanachama wetu ili lipigiwe kura."

Kansela Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture alliance/dpa/b. von Jutrczenka

Bado hakujatolewa taarifa zaidi kuhusiana na mkutano huo wa wiki ijayo, ila Merkel siku zote amekuwa akisema kwamba yuko tayari kwa mazungumzo.

Kuiunga mkono serikali kunaweza kuwa kwa njia nyingi mbali na kuundwa kwa serikali ya mseto, mojawapo ya njia hizo zikiwa kukubali kwa njia rasmi kutoipinga serikali ya wachache inayoongozwa na Merkel au kukubali kuiunga mkono serikali hiyo kwa njia isiyo rasmi.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/APE

Mhariri: Mohammed Khelef