Schumacher kustaafu Formula 1
23 Novemba 2012Schumacher ataendesha gari la Formula One kwa mara ya mwisho Jumapili hii katika mkondo wa Brazil Grand Prix. Schumacher anashikilia rekodi karibu zote za Formula One, ikiwa ni pamoja na ushindi 91 wa Grand Prix na kupata nafasi za kwanza 68 pamoja na mataji saba ya ubingwa wa F1 akiwa na timu za Benetton na Ferrari. Awali baada ya kustaafu mwishoni mwa mwaka wa 2006, alirejea tena katika mwaka wa 2010 na timu ya Merecedes, lakini katika awamu yake ya pili katika mashindano ya F1 hajaweza kuongeza mataji mengine na nafasi yake itachukuliwa msimu ujao na Lewis Hamilton. Mkufunzi wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew anasema Schumacher ni jina maarufu kispoto kote ulimwenguni siyo tu nyumbani Ujerumani. Mafanikio yake katika F1 yanajieleza yenyewe na kamwe hayatasahaulika.
Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani Michael Ballack anasema Schumacher ni mmoja wa wanaspoti maarufu katika miongo iliyopita. Pia familia ya F1 imemsifu dereva huyo huku Kiongozi wa Ferrari Stefano Domenicali akisema jina la Schumacher limehusishwa na takribani nusu ya ushindi wa timu yake na atasalia mioyoni mwa familia ya Ferrari. Rais wa Mercedes Ross Brawn ambaye amewahi kufanya kazi na Schumacher kwa muda mwingi wa taalum yake amesema mbio za kesho nchini Brazil zitakuwa na huzuni kwa kila mtu katika kikosi chao.
Benitez afurahia kazi ya Chelsea
Kaimu mkufunzi mpya wa Klabu ya Chelsea Rafael Benitez amesema changamoto ya kujaribu kushinda mataji matano msimu huu ilikuwa ni fursa kubwa kwake kukataa wakati aliporejea katika Ligi ya Premier Alhamisi wiki hii.
Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 52, ambaye aliondoka Liverpool mwishoni mwa msimu wa 2009-2010 na kuchukua nafasi ya Roberto Di Matteo uwanjani Stamford Bridge, kwamba ana furaha kujiunga na Chelsea na haijalishi kama ni mkataabw a muda mfupi au muda mrefu. Cha muhimu anasema ni kushinda mechi baada ya nyingine na kisha kutwaa mataji...
Pamoja na Premier League, mabingwa hao wa Ulaya bado wanashiriki katika Ligi ya Mabingwa ijapokuwa wanachungulia kaburi na ni muujiza wakifuzu katika awamu ya mchujo. Pia wanashiriki katika Kombe la Shirikisho, huku harakati za kutetea kombe la FA zikianza mwezi Januari, mwezi mmoja baada ya kushiriki katika kinyang'Anyiro cha Kombe la Klabu Bingwa Ulimwenguni.
Maafisa wakuu wa soka ya Uingereza sasa wataanza kurkodi mawasiliano wakati wa mechi kufutia kesi iliyomkabili Refarii Mark Clattenburg. Wakuu wa waamuzi wanalenga kuepuka marudio ya tukio kama hilo, baada ya Clattenburg kuondolewa madai na Shirkisho la Soka Uingereza FA, kwamba alimtolea matamshi ya kibaguzi kuungo wa Chelsea Mnigeria John Obi Mikel, baada ya uchunguzi wa muda mrefu kukosa kupata ushahidi wa kuwepo makosa yoyote.
Kwa sasa maafisa wa mechi katika ligi ya Premier, waamuzi wasaidizi na afisa wa nne, wote wana vifaa vya kusikiliza na kuzungumza ili kuwasaidia kuwasiliana vyema wakati kuna makelele uwanjani, lakini mazungumzo yao awali hayajakuwa yakirekodiwa.
Wakati huo huo, refarii Mark Clattenburg atajitosa uwanjani tena kutekeleza majukumu yake kuanzia kesho atakapoongoza mechi kati ya Tottenham Hotspurs dhidi ya Westham, na kisha asimamie mchuano wa Jumatano kati ya Southampton na Norwich katika uwanja wa St.Mary's.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman