semenya kubeba bendera ya Afrika kusini
27 Julai 2012Semenya mwenye umri wa miaka 21 alipewa fursa hiyi hivi karibuni. Mwogeleaji Cameron Van der Burgh na mrukaji Khotso Mokoena pia walikuwa katika ile orodha ya watu waliochaguliwa na kamati ya Olimpiki.
Semenya alisema kuwa ni fursa ya kiheshima kwake kufanya alichokiita kitu kikukubwa cha kubeba bendera ya taifa kwa niaba ya timu itakayoiwakilisha Afrika Kusini.
Msimamizi mkuu katika kamati ya Olimpiki ya Afrika Kusini, Tubby Reddy alisema kuwa walikuwa wakimfikiria pia mwanariadha Pistorius ambaye atafanya jambo la kihistoria kwa kuwa kuwa mlemavu wa kwanza kukimbia katika michezo ya Olimpiki baada ya kutajwa katika dakika za lala salama kuwa ni miongoni mwa watakaojiunga timu ya Afrika Kusini katika mashindano hayo.
Tubby Reddy alisema kuwa kulikuwa na wanariadha wachache waliotarajia kuibeba bendera hiyo mjini London kwa hivyo walimchagua Semenya. Aliongeza pia kuwa amekuwa mshindi wa dunia na wanatarajia kuwa atashinda medali ya dhahabu katika Olimpiki mwaka huu. Tubby aliongeza kuwa iwapo wangemchagua Oscar Pistorius basi kungetokea maswala mengine.
Semenya, ambaye ni mshindi wa zamani katika mbio za mita 800 na aliyeshinda medali ya fedha mwaka uliopita hakuhudhuria sherehe ya kuwaaga rasmi timu ya kuiwakilisha taifa hilo kwa vile alikuwa Monaco ambako anafanya matayarisho ya mwisho kabla ya mashindano ya Olimpiki huko London. Aliikubali fursa hiyo ya kubeba bendera ya Afrika kusini kupitia ujumbe uliorekodiwa. Natalie du Tout, mwogeleaji wa Olimpiki ndiye alieibeba bendera hiyo mwaka 2008 katika mashindano ya michezo ya Beijing.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Semenya kushindana katika Olimpiki. Miaka mitatu iliyopita alikumbwa na tetesi za kuthibitiwa kwa jinsia yake kufuatiwa na ushindi wake mkubwa mjini Berlin, Ujerumani. Semenya alilalamika kuwa kutakiwa kwa thibitisho la jinsia yake sio muhimu na kuwa itakuwa uvamizi wa faragha yake.
Alitengwa kwa miezi 11 wakati shirika la IAAF ilikuwa ikihakiki majaribio ya jinsia yake na kukubaliwa kurudi katika mashindano mwaka 2010 lakini hangeweza kushindana kwa sababu ya maumivu ya mgongo. Mwaka uliopita alimaliza wa pili katika mbio za mita 800 kule South korea licha ya kuhangaika na maumivu hayo.
Aidha, Semenya aliwaambia waandishi wa habari wa Ulaya kuwa jinamizi hilo ameliacha nyuma na kuwa ana matarajio ya kushinda dhahabu katika Olimpiki ambayo akipata atakitunukia Nelson Mandela ambaye ni mwanasiasa maarufu wa Afrika kusini.
Semenya anakumbuka wakati wake wa kwanza kukutana naye Nelson Mandela alikuwa msichana mdogo tu. Lakini Nelson Mandela alikuwa na imani kwake. Kwa hivyo chochote anachokifanya ni kwa ajili yake Mandela kwa vile yeye humtia moyo.
Caster Semenya ambaye rekodi yake ya muda mfupi zaidi ni dakika 1.59 na sekunde 18 amewai kushindwa mara 5 na mshindi wa Olimpiki ya mwaka 2008 na Mkenya Pamela Jelimo. Lakini anasema kuwa anaangalia mbele. Kila mwaka anazidi kuwa mwanariadha bora kwa hivyo mashindano haya yatakuwa ya nia thabiti kwake.
Mwandishi : Trizer Ochieng/AFPE
Mhariri: Sudi Mnette