1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Senegal yafunga shule za Fethullah Gulen

18 Machi 2018

Serikali ya Senegal imezifunga shule zaidi ya 12 zinazomilikiwa na mtu ambaye serikali ya Uturuki inamchukulia kuwa gaidi, na kutilia mkazo kuzidi kwa ushawishi wa Uturuki katika kanda ya Afrika Magharibi.

https://p.dw.com/p/2uY5Q
Fethullah Gülen
Mhubiri wa Kituriki Fethullah Gulen, ambaye serikali ya Uturuki inamtuhumu kwa kupanga njama ya mapinduzi iliyoshindwa Julai 2016.Picha: picture alliance/dpa/M.Smith

Karibu wanafunzi 3,000 nchini Senegal wameathirika katika harakati za Uturuki kupunguza ushawishi wa Fethullah Gulen, ambaye anatajwa kuwa gaidi na serikali ya Uturuki.

Shule zilizofungwa mwaka jana zilikuwa zinafungamanishwa na vuguvugu la Hizmet, ambalo lilijengwa kwa msingi wa mafundisho ya Gulen, kiongozi wa kidini wa Uturuki anaeishi uhamishoni nchini Marekani, na anatuhumiwa na serikali Uturuki kwa kupanga njama ya mapinduzi mwaka 2016.

Suala hilo limepata umuhimu katika kanda ya Afrika Magharibi kufuatia ziara ya karibuni ya rais wa Uturuki. Karibu mataifa 30 yameathirika barani Afrika.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alizitembelea Algeria, Mauritania, Senegal na Mali, na kukutana na wakuu wa nchi hizo akiambatana na ujumbe wa viongozi wa kibishara wa Uturuki kuongeza uwekezaji barani Afrika. Erdogan alizishukuru nchi hizo kwa kuzifunga shule zinazohusiana na Gulen.

Algerien Afrikareise des türkischen Präsidenten Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alipokutana na mwenzake wa Algeria Abdelaziz Bouteflika, wakati wa ziara ya Erdogan nchini humo, ambayo ilimpeleka pia Afrika Magharibi.Picha: picture-alliance/dpa/AP Images/Pool Presidential Press Service/K. Ozer

"Nchi nyingi zilizorubuniwa na shirika la kigaidi la Gulen zilikuwa barani Afrika," Erdogan alisema mwanzoni mwa ziara yake ya wiki nzima. Shule za nchini Gambia, Guinea, Somalia, Chad, Mauritania, Niger, Gabon, Senegal na sasa Mali zimehamishiwa kwenye wakfu wa serikali yake wa Maarif, alisema.

Ushawishi wa Gulen barani Afrika

Nchini Senegal, Wakfu wa Maarif ulifungua shule tatu mpya. Gulen alikuwa na ushawishi mkubwa nje ya Uturuki: Ripoti ya idara ya upelelezi ya Uturuki inasema Mtandao wa Gulen ulikuwa na shule karibu 2,800, taasisi za elimu, wakfu, mashirika yasiyo ya kiserikali na hospitali katika matafa karibu 170.

Kufungwa kwa shule barani Afrika kutatazamwa nchini Uturuki kama hatua chanya katika mapambano dhidi ya Guleni, alisema Emre Caliskan, mtafiti katika chuo kikuu cha Oxford anaejikita katika uhusiano wa Uturuki na Afrika.

Lakini shule ni sehemu tu ya juhudi za Uturuki kuimarisha uwepo wake barani Afrika. Uturuki imeongeza idadi ya balozi zake barani Afrika kutoka 12 mwaka 2003 hadi 41 hivi sasa. "Uturuki inahitaji msaada wa mataifa ya Afrika katika Umoja wa Mataifa," alisema Caliskan.

Murat Kadir, mratibu wa Wakfu wa Maarif nchini Senegal, alisema ni baadhi tu ya wanafunzi waliokuwa katika shule za zamani za Gulen wamehamishiwa katika shule tatu mpya zilizofunguliwa na wakfu huo mwezi Novemba 2017 ambapo wanafunzi karibu 120 wako nchini Senegal. Wanapanga kuongeza zaidi, alisema.

Senegal Schulklasse in Dakar
Darasa la shule katika mji mkuu wa Senegal, Dakar.Picha: DW/M. lamine Ba

Wanafunzi waliobakia kati ya wale 3,000 ambao shule zao zilifungwa nchini Senegal walipaswa kutafuta taasisi nyingine.

Fady Ndao, ambaye binti yake wa miaka 16 alisoma katika shule ya Gulen, ya College Sultan kabla ya kufungwa, alisema alichagua kumpeleka katika shule ya serikali badala ya kumhamishia kwenye shule mpya ya serikali ya Uturuki mjini Dakar.

"Ikiwa ni kwa sababu za kisiasa, hilo siyo sahihi," alisema kuhusu kufungwa kwa shule za Gulen. "Sisi ni Wasenegali nchini Senegal. Tuna haki ya kuchaguwa elimu nzuri tukiwa hapa."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri. Sylvia Mwehozi