Senegal yaliokoa bara la Afrika kombe la dunia
20 Juni 2018Baada ya Nigeria na Algeria ambazo zote zilifikia awamu ya mtoano miaka minne iliyopita, baada ya Ghana kufikia robo fainali mwaka 2010, tayari inaonekana kama mwaka 2018 kuwa ni hatua moja nyuma kwa bara la Afrika katika medani ya juu kabisa ya soka duniani.
Kufuatia hamasa kubwa ya kuwakilishwa kwa mara ya kwanza katika fainali hizi tangu mwaka 1990, Mafaraoh wamejikuta wakiutumbulia macho mlango wa kutoka baada ya siku sita za mashindano haya.
Kikosi cha Hector Cuper kimeathirika na matatizo ya kiafya ya Mohamed Salah, ambaye hakushiriki katika kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Uruguay mjini Yekaterinburg.
Jana Jumanne(19.06.2018), Salah alirejea katika kikosi hicho lakini alishindwa kuzuwia Misri kupokea kipigo kingine mara hii mabao 3-1 dhidi ya Urusi mjini Saint Petersburg, mkwaju wake wa penalti katika dakika za mwisho ukiwa kama la kufutia machozi.
"Ni vigumu mno kutambua kile ambacho kingetokea ( iwapo asingekuwa majeruhi) lakini tunafahamu uwezo wake," alisema kocha Cuper.
Misri bado haijashinda mchezo wake katika fainali za kombe la dunia katika mara sita za kujaribu. Ni Honduras pekee ambayo imejaribu mara tisa ilicheza michezo mingi zaidi katika fainali za kombe la dunia bila ya kupata ushindi wowote, na Mafaraoh wanafahamu kwamba sare kwa Uruguay dhidi ya Saudi Arabia siku ya Jumatano jioni itashuhudia wakienguliwa katika mashindano haya.
Morocco waishiwa nguvu
Kikosi cha Herve Renard wa Morocco hakikuwahi kufungwa bao hata moja wakati wa kufuzu kucheza katika fainali hizi katika kundi lao barani Afrika. Na ilikuwa bao la dakika za mwisho la kujifunga la Aziz Bouhaddouz lililosababisha kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Iran katika mchezo wao wa ufunguzi.
Walianza mchezo huo vizuri sana , wakianza kwa kuwabana wachezaji wa Iran wakiwa langoni mwao, (pressing), wakati Amine Harit akicheza vizuri sana. Lakini waliishiwa nguvu na wamebakiwa na mchezo dhidi ya Ureno ya Cristiano Ronaldo na Uhispania kujaribu kuokoa kampeni yao, hali ambayo ni ngumu.
"Hatuna muda wa kusikitika," amesema Renard, na hata kama Morocco itayaaga mashindano na mapema, matumaini ni kwamba hii itakuwa eneo la kujifunza kwa wachezaji chipukizi wenye kipaji.
Kikosi cha tai wa kijani cha kocha Gernot Rohr walifanya vibaya wakati walipoanza kampei kwa kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Croatia mjini Kaliningrad katika kundi gumu, ambalo pia lina timu za Argentina na Iceland.
Goli la kujifunga la Oghenekaro Etebo na penalti iliyopigwa na Luka Modric iliifanya Nigeria hata kutotambulika tena kutoka timu ile iliyofungwa na Ufaransa katika awamu ya timu 16 zilizosalia katika fainali za kombe la dunia miaka minne iliyopita.
"Baadhi ya nyakati tulikuwa hatujielewi kunapotokea mipira ya adhabu lakini tutaifanyia kazi," amesema Rohr, ambaye timu yake itapabambana na Iceland.
Kocha wa Tunisia Nabil Maaloul amesisitiza kwa kujiamini kabla ya fainali hizi za kombe la dunia kwamba kikosi chake kitafuzu kuingia katika awamu ya mtoano kutoka katika kundi ambalo lina timu za Ubelgiji na Uingereza na karibu wangekilazimisha kikosi cha kocha Gareth Southgate kutoka sare mjini Volgograd katika mchezo wao wa kwanza.
Walirejea mchezoni baada ya kukubali bao la mapema na walimpoteza mlinda mlango Mouez hassen kutokana na kuumia, na wakasawazisha kwa mkwaju wa penalti wa Ferjani Sassi.
Baada ya kuona timu nyingine za Afrika zikipata kibarua kigumu, Senegal ilifanya wajibu wake kwa kupambana kiume na kutoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Poland jana Jumanne (19.06.2018) katika kundi H.
Mwandishi: Sekione Kitojo