1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Senegal yatinga fainali ya AFCON kwa kuichapa Burkina Faso

Sylvia Mwehozi
3 Februari 2022

Senegal wamefanikiwa kutinga fainali ya michuano ya kombe la mataifa ya Afrika kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kuitandika Burkina Faso bao 3-1

https://p.dw.com/p/46RJh
Africa Cup of Nations | Burkina Faso v Senegal
Picha: MOHAMED ABD EL GHANY/REUTERS

Wachezaji Abdou Diallo, Idrissa Gana Gueye na Sadio Mane ndio waliopachika magoli katika kipindi cha pili cha mchezo na kuifanya Senegal kuibuka na ushindi.

Timu ya Senegal inayonolewa na kocha Aliou Cisse ilipewa mikwaju miwili ya penalti katika kipindi cha kwanza, kabla ya mwamuzi wa kutoka Ethiopia kubadili mawazo yake kufuatia tathmini ya VAR. Hata hivyo, Senegal, walipambana na katika kipindi cha pili mshambuliaji anayekipiga klabu ya Paris Saint-Germain PSG Diallo alipachika bao la kwanza.

Bao la pili lilipatikana dakika ya 76 wakati Sadio Mane alipotoa pasi safi kwa Guaye ambaye pia anakipiga klabu ya PSG. Mane alihitimisha ushindi wa Senegal kwa kupachika bao la tatu.

Africa Cup of Nations | Burkina Faso v Senegal
Mambo yalivyokuwa katika mchezo wa nusu fainali baina ya Senegal na Burkina FasoPicha: KENZO TRIBOUILLARD/AFP/Getty Images

"Tulijua isingekuwa rahisi, ilikuwa ni nusu fainali ya Kombe la Mataifa," alisema Mane akiongeza kuwa "tulikuwa tunapambana na timu nzuri ya Burkina Faso ambayo ilitupa changamoto kubwa. Tulikuwa watulivu na tulitumia nafasi zetu na nadhani tulistahili ushindi huu."

Senegal ambayo inashikilia nafasi ya kwanza katika viwango vya soka barani Afrika, itasubiri kufahamu mpinzani wake katika mchezo wa pili wa nusu fainali baina ya Misri na Cameroon utakaopigwa baadae leo. 

Misri na Cameroon ni nchi mbili zenye mafanikio makubwa katika historia ya mashindano ya AFCON, Misri ikiwa ni mabingwa mara saba na Cameroon wameshinda kombe mara tano. Timu ya Senegal ama ikijulikana zaidi kama Simba wa Teranga wanatafuta kushinda kombe hilo, miaka miwili baada ya kupoteza dhidi ya Algeria katika fainali ya mjini Cairo.

Nani sasa ataelekea nusu fainali AFCON?

Burkina Faso wamejidhihirisha kuwa timu yenye vipaji chipukizi na wakiwa na shauku ya kuwapatia furaha mashabiki zao nyumbani, hasa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya wiki iliyopita. Mapinduzi hayo yalitokea wakati timu ya taifa ikiendelea na mashindano.

Mwamuzi Bamlak Tessema, awali alitoa ishara ya penalti kwa Senegal kabla ya kubadili mawazo baada ya kuitizama VAR. Penalti nyingine ilitolewa dakika za majeruhi kipindi cha kwanza wakati shuti la Gueye lilipogonga mkono wa Edmond Tapsoba wa Burkina Faso katika eneo lao, lakini tena mwamuzi alibadili mawazo baada ya kuitizama VAR.

Wakati huohuo shirikisho la soka afrika CAF, limesema mechi ya kuwania nafasi ya tatu ya Kombe la Mataifa ya Afrika itachezwa Jumamosi hii, Februari 5. Awali mechi hiyo ilikuwa imepangwa kufanyika saa tatu kabla ya mchezo wa fainali siku ya Jumapili, lakini sasa itachezwa Jumamosi saa 8:00 mchana.

CAF imeongeza kuwa kucheza mechi hizo mbili siku ya Jumapili kungesababisha matatizo kwa vikosi vya usalama katika mji mkuu wa Cameroon na maafisa wa CAF wasingeweza kusambaza medali kwa timu iliyoshika nafasi ya tatu na kisha kuelekea uwanja wa mechi ya fainali, uliopo umbali wa takriban kilomita 12, kwa wakati.