1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera za Ufaransa zaigeuza muhanga wa mashambulizi

Mohammed Khelef15 Julai 2016

Baada ya mashambulizi mawili yaliyouwa watu 17 mjini Paris mwezi Januari 2015, gazeti la Dar al-Salaam linalomilikuwa na "Dola la Kiislamu" (IS) lilichapisha Mnara wa Eifell likiandika "Allah ilaani Ufaransa."

https://p.dw.com/p/1JPgT
Muombolezaji akibeba uwa la huzuni katika mji wa Nice, Ufaransa.
Muombolezaji akibeba uwa la huzuni katika mji wa Nice, Ufaransa.Picha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Ufaransa ilivamiwa tena mwezi Novemba na watu 130 kuuawa kwa mashambulizi ya mabomu na bunduki, na sasa mashambulizi ya Nice yameangamiza watu 84, baada ya dereva wa lori kuuvamia umati uliokuwa ukiangalia maonesho ya fashifashi jioni ya Alhamis (Julai 14), kama sehemu ya Sikukuu ya Kitaifa.

"Ugaidi ni kitisho kinachoielemea Ufararansa na kitaendelea kuwa hivyo kwa muda mrefu," alisema Waziri Mkuu Manuel Valls, siku ya Ijumaa akiapa kuwa serikali yake italipiza kisasi.

Mkuu wa kikosi cha kupambana na ugaidi cha Ufaransa, Patrick Calvar, alisema maneno kama hayo kwenye kikao cha kamati ya bunge mwezi Mei, ambapo wakati huo wasiwasi mkubwa ulikuwa ni usalama kwenye michuano ya Euro2016. Hatimaye, mashindano hayo yalimalizika salama usalimini.

"Leo, Ufaransa ni moja ya nchi zinazotishiwa sana kabisa," alisema mkuu wa Kurugenzi Kuu ya Usalama wa Ndani (DGSI). "Suala kuhusiana na kitisho hiki sio jinsi ya kujuwa kuwa kipo ama la, lakini ni lini na wapi yatafanyika mashambulizi."

Sababu za Ufaransa kuandamwa

Kwa mujibu wa propaganda ya IS, sababu zinazoifanya Ufaransa kuwa mlengwa mkuu wa makundi ya siasa kali zinaanzia kwenye operesheni za sasa za kijeshi za nchi hiyo na kurudi nyuma hadi kwenye Vita vya Msalaba vya karne za 11 mpaka 15 wakati huo Wakristo wakipambana na Waislamu kwenye Mashariki ya Kati.

Waombolezaji wakiweka maua kuomboleza mauaji ya Nice, Ufaransa.
Waombolezaji wakiweka maua kuomboleza mauaji ya Nice, Ufaransa.Picha: DW/B. Riegert

Ufaransa, ambayo ndiyo yenye idadi kubwa kabisa ya Waislamu barani Ulaya, ina pia utamaduni mkali wa kidola unaoitenga dini kando kabisa na maisha ya kawaida, ikiwemo sheria isiyo mashuhuri ya kupiga marufuku uvaaji wa burka na vilemba katika skuli za umma na ofisi za serikali.

Waungaji mkono wa sheria hizo wanasema zinashajiisha utambulisho wa pamoja wa Kifaransa, lakini wakosoaji wanasema inazitenga jamii zisizokuwa za Kikristo, ambao wanashuhudia sikukuu nyingi rasmi za Kikatoliki zikiwa za kitaifa kama vile Krisimasi na Pasaka, lakini kwao kukiwa hakuna chochote kinachoheshimiwa.

Operesheni za Kijeshi

Baada ya mashambulizi ya Paris, IS waliweka wazi kuwa Ufaransa na mataifa mengine yanayopambana nao yataendelea kuwa walengwa wakubwa, madhali tu yanaendeleza "vita vya msalaba" nchini Syria na Iraq.

Ufaransa inafanya mashambulizi ya naga na operesheni maalum dhidi ya kundi hilo na inatoa mafunzo kwa wanajeshi wa Kikurdi na wa Iraq nchini Iraq. Akizungumzia mashambulizi ya Nice, Rais Francoise Hollande aliapa kuongeza kampeni hiyo ya kijeshi dhidi ya IS.

"Ufaransa imetanzwa na chuki za kipumbavu dhidi ya Uislamu na Waislamu ambazo ziliipelekea kuwa kiongozi wa muungano wa vita dhidi ya ukhalifa," liliandika gazeti la Dar al-Islam mwaka jana, ikikusudia maeneo yanayokaliwa na IS nchini Syria na Iraq.

Lakini Ufaransa pia ina vikosi vyake katika mataifa ya magharibi mwa Afrika, ambako vinasaidia kuwasambaratisha wapiganaji wenye siasa kali. Mwaka 2011, ilichukuwa uongozi katika mashambulizi ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO dhidi ya serikali ya Muammar Gaddafi wa Libya, ambako waasi walikuwa wakipigana kuiangusha serikali hiyo.

Dhima hii ya Ufaransa kwenye Mashariki ya Kati na Afrika inarejea nyuma kwenye historia yake ya ukoloni kwenye maeneo hayo, na mashambulizi ya kulipiza kisasi ndani ya ardhi ya Ufaransa yanarudi nyuma kwenye Vita vya Algeria kati ya mwaka 1954 hadi 1942.

Sera za Ndani

Ikiwa na sera kali ambazo zinaweka mipaka ya uonekanaji wa dini kwenye maeneo ya umma, Ufaransa ina sera za ndani ambazo zinawakasirisha Waislamu wenye siasa kali. Baadhi ya watu miongoni mwa Waislamu milioni tano wa nchi hiyo, ambao ni asimilia nane ya Wafaransa wote, wanalalamikia ubaguzi na wengi wao wanaishi kwenye maeneo ya kimasikini katika miji mikubwa.

Waombolezaji nchini Austria wakiomboleza mauaji ya Nice, Ufaransa.
Waombolezaji nchini Austria wakiomboleza mauaji ya Nice, Ufaransa.Picha: Reuters/D. Gray

Hawa wanaona kuwa Ufaransa imekuwa katili sana kwao na kwa dini yao. Kwa mfano, skuli nyingi za umma zimekataa kutoa chakula cha halali kwa Waislamu, zikidai kuwa taifa hilo halina dini.

Kuna jambo jengine pia. Ufaransa ina utamaduni mkongwe kabisa wa shitihizai, ambao unaingia mpaka kwenye masuala ya kidini, nayo ilikuwa moja ya sababu za Waislamu wenye siasa kali kuzishambuliwa jarida la Charlie Hebdo mwaka jana na kuuwa watu 12.

Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Ugaidi, Calvar, aliashiria tatizo hasa lililopo wakati Ufaransa ikipambana na ugaidi kuwa ni mshangao ambao huwakumba. Mwezi Mei, kwa mfano, wasiwasi wao mkubwa ni kuwa bomu lingetegwa kwenye mikusanyiko ya watu wanaotazama mechi za Euro2016, lakini hilo halikutokezea, na badala yake ikatumika mbinu ya kuendesha lori na kuwaponda watu, mbinu ambayo hata haikuwahi kufikiriwa na mamlaka za ulinzi na usalama.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga