1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera za vyama vikuu vya kisiasa zakosolewa Ujerumani

Oumilkheir Hamidou
12 Februari 2018

Makubaliano ya kuunda serikali mpya ya muungano wa vyama vikuu kati ya wahafidhina wa CDU/CSU na wana Social Democrat wa SPD yamezusha malalamiko. Sauti zinahanikiza kudai wazee wakae kando na kupewa nafasi vijana

https://p.dw.com/p/2sVTw
SPD-Sonderparteitag Martin Schulz und Andrea Nahles
Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Chama cha Social Democrat kimezama katika bahari ya misuko suko. Shinikizo la ndani limepelekea Martin Schulz aliyekusudiwa wadhifa wa waziri wa mambo ya nchi za nje katika serikali kuu mpya ya muungano atangaze kujitoa serikalini. Na hatima ya kaimu waziri wa mambo ya nchi za nje Sigmar Gabriel nayo pia haijulikani.

Naibu mwenyekiti wa chama cha Social Democrat Ralf Stegner ametoa wito wa kurejeshwa nidhamu na kumalizika mjadala kuhusu nani akabidhiwe wadhifa gani chamani."Tangazo la kujiuzulu mwenyekiti wa chama Martin Schulz, nyadhifa zake zote na mijadala kuhusu nani akabidhiwe wadhifa upi ni onyo la mwisho kwa chama chake" amesema Ralf Stegner katika mahojiano kupitia kituo cha pili cha televisheni ya Ujerumani ZDF:"Masuala kuhusu wanaostahiki kukabidhiwa nyadhifa serikalini na chamani hatuwezi kuyapatia jibu haraka haraka.Tunabidi na tunataka kwanza tushughulikie masuala ya kimsingi yaliyomo ndani ya makubaliano ya kuunda serikali."Ameongeza kusema.

Mwenyekiti wa tawi la vijana wa SPD Jens Kühnert apania kuona makubaliano ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu yanapingwa na wanachama wa SPD
Mwenyekiti wa tawi la vijana wa SPD Jens Kühnert apania kuona makubaliano ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu yanapingwa na wanachama wa SPDPicha: picture-alliance/dpa/S. Willnow

Kamati kuu ya SPD kukutana kesho jumanne

Makamo mwenyekiiti wa SPD, Stegner amesema wameshangazwa na uamuzi wa Martin Schulz wa kujiuzulu. Kuhusu suala kama mwenyekiti mpya achaguliwe kupitia kura ya wanachama, Ralf Stegner anasema hilo ni miongoni mwa mageuzi yaliyopendekezwa. Kamati kuu ya SPD imepanga kukutana kesho na huenda ikamteuwa mkuu wa kundi la wabunge wa SPD, Andrea Nahles aliyependekezwa  hapo awali na Martin Schulz, kuwa mwenyekiti wa muda wa SPD.

Katibu mkuu wa SPD Lars Klingbeil anaunga mkono pendekezo la kuteuliwa Andrea Nahles ,mwenye umri wa miaka 47 kuwa pia mwenyekiti wa SPD.

Kansela Angela Merkel
Kansela Angela MerkelPicha: Reuters/H. Hanschke

CDU pia kinalaumiwa na wanachama wake

Malalamiko ya nani akabidhiwe wadhifa gani yanahanikiza pia katika chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union-CDU cha kansela Angela Markel.Tawi la vijana wa chama hicho wameweka muda wa hadi mwisho wa mwezi huu, utakapoitishwa mkutano mkuu, wapatiwe jibu la suala akina nani miongoni mwa wana CDU, watakabidhiwa nyadhifa za mawaziri katika setikali mpya ya muungano wa vyama vikuu-GroKo. Vijana wa CDU wanataka vijana wapewe nafasi zaidi katika serikali mpya. Katika mahojiano kupitia kituo cha Televisheni cha ZDF jana usiku, kansela Angela Merkel ametetea uamuzi wa kuwakabidhi, SPD wizara muhimu ya fedha. Kuhusu kukabidhiwa vijana nyadhifa serikalini kansela Merkel amesema majina ziada yatajulikana mkutano mkuu wa chama utakapaoitishwa february 26 inayokuja.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa/

Mhariri: Mohammed Khelef