1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yatakiwa kuondoa sheria zinazokandamiza uhuru wa kutoa maoni

30 Juni 2016

Wakati serikali ya Myanmar inayoongozwa na chama cha mwanaharakati wa haki za binadamu Aung San Suu Kyi cha National League for Democracy (NLD) ikifikisha siku mia moja, na kutakiwa kuondoa sheria kandamizaji.

https://p.dw.com/p/1JGbv
Kiongozi wa chama cha NLD nchini Myanmar Aung San Suu Kyi akiwa bungeni..
Kiongozi wa chama cha NLD nchini Myanmar Aung San Suu Kyi akiwa bungeni..Picha: picture alliance/dpa/H. Htet

Hatua hiyo inafuatia ripoti iliyotolewa hapo jana na Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch ambayo inaonyesha sheria inayohusu mawasiliano na kukashifu, imetumika kuwatia mbaroni watu 70 katika kipindi cha mwezi mmoja.

Kukamatwa kwa watu hao kunafanyika licha ya mageuzi yaliyofanywa na Rais wa zamani wa nchi hiyo Thein Sein na chama cha NLD,ambacho kilishinda uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka jana kwa asilimia kubwa na hivyo kupata nguvu ya kudhibiti mabunge yote ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kumpa nafasi mwanaharakati za haki za binadamu Aung San Suu Kyi kuiongoza nchi hiyo.

"Tunafikiri kwamba kumekuwa na mafanikio kadhaa ambayo yameletwa na serikali hii mpya" amesema David Mathieson, ambaye ni mtafiti mwandamizi katika Shirika la Human Rights Watch, akimaanisha juhudi ambazo tayari zimefanywa na chama cha NLD za kufanya marekebisho ya sheria ambazo zimekuwa zikibana uhuru wa kutoa maoni.

Chama cha NLD nchini Myanmar chastahili pongezi

Aidha mtafiti huyo amesema licha ya chama hicho cha NLD kusitahili pongezi kutokana na hatua ambayo tayari chama hicho kimechukua kwa kuwaachia huru wafungwa wengi wa kisiasa bado kuna sheria ambazo zinakandamiza uhuru huo wa kutoa maoni ambazo nazo zinatakiwa kuondolewa.

Wafuasi wa chama cha NLD nchini Myanmar .
Wafuasi wa chama cha NLD nchini Myanmar .Picha: DW/Patrick Benning

Chama cha NLD ambacho kinaundwa na wanaharakati pamoja na wapinzani kisiasa kimeziondoa sheria kadhaa za kikandamizaji na kupendekeza sheria nyingine zifanyiwe marekebisho kama vile sheria ya kukusanyika ambayo inaruhusu kuwepo kwa maandamano ambayo awali yalipigwa marufuku na serikali iliyokuwa ya kijeshi lakini bado sheria hiyo inaweka mipaka na inatumika kukamata na kuwatia jela waandamani wengi.

Mapendekezo ya marekebisho ya sheria yaliyotolewa na NLD ni hatua moja wapo ya mafanikio. Imesema Human Rights Watch .

Muswada huo wa marekebisho ya sheria hiyo ambao unajadiliwa katika bunge la nchi hiyo, endapo utapitishwa utawabana na kuwatia hatiani waandamanaji ambao watapatikana na makosa ya kusambaza kile inachokitaja kuwa ''habari za uwongo''.

Kwa mujibu wa Human Rights Watch sheria nyingine ambayo inaleta usumbufu ni sheria ya mawasiliano ambayo inazuia matumizi ya mitandao ya mawasiliano kufanya mambo inayoyataja kuwa ni ''kutisha, kukashifu au kusababisha usumbufu'' na vitendo vingine vinavyofanana na hivyo.

Kukamatwa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamiii ambao ujumbe wao katika mitandao hiyo unaochukuliwa kuwa kinyume cha maadili na kisheria vimekuwa vikiendelea chini ya serikali ya Suu Kyi.

Hata hivyo kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Human Rights Watch suala la kuleta mageuzi katika sheria kadhaa nchini Myanmar bado ni changamoto kubwa.

Mwandishi : Isaac Gamba / RTRE

Mhariri : Gakuba Daniel