1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali mpya ya Palestina yakutana.

Mohamed Dahman18 Juni 2007

Baraza la mawaziri la dharura la Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Palestina limekutana kwa mara ya kwanza leo hii tokea kundi la Hamas lilipochukuwa kwa umwagaji damu Ukanda wa Gaza huku kukiwa na ishara kwamba vikwazo vya mataifa ya magharibi vilivyodhoofisha mamlaka ya Palestina yumkini vikaondolewa hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/CHCY
Waziri Mkuu mpya wa Mamlaka ya Palestina Salam Fayyad.
Waziri Mkuu mpya wa Mamlaka ya Palestina Salam Fayyad.Picha: AP

Waziri Mkuu mpya wa Mamlaka ya Palestina Salam Fayyad mwanauchumi aliesomea Marekani alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo wa takriban masaa mawili wa baraza la mawaziri 12 katika mji mkuu wa kisiasa wa Ukingo wa Magharibi wa Ramallah na kutowa ahadi za kuondowa mgawanyiko wa Wapalestina.

Waziri wa habari Riyad al Malki amewaambia waandishi wa habari kwamba watachukuwa hatua ya kurekebisha hali hiyo isio ya kawaida kwa kuona kwamba hatua kwa hatua zinachukuliwa kukomesha hali hiyo katika Ukanda wa Gaza.

Amesema Mamlaka ya Palestina inaendelea kubakia huko Gaza kadhalika katika Ukingo wa Magharibi na kwamba inawajibika kiiutawala na kimaadili kwa watumishi wote wa serikali,raia na jeshi.

Awali akizungumza kufuatia kuapishwa kwa baraza hili jipya la mwaziri Saeb Arakat mshirika wa karibu wa Rais Abbas alisema hawana serikali mbili wana serikali moja rasmi inayoongozwa na Salam Fayyad na kwamba kile kinachotokea Gaza hivi sasa ni hali ya hatari na hali hiyo iko nje ya uwezo wao.

Abbas akiungwa mkono na jumuiya ya kimataifa ameliapisha baraza jipya la mawaziri hapo jana na kwa haraka akatunisha misuli yake kwa kupiga marufuku vikosi vya ulinzi vya Hamas na kuvunja baraza la usalama la taifa ambalo linajumuisha viongozi wa itikadi kali za Kiislam wa Hamas.

Hamas mashirika mkuu katika serikali ya umoja wa kitaifa iliotimuliwa imeipuuza serikali hiyo mpya yenye makao yake Ukingo wa Magharibi kuwa sio halali na kwamba ni kibaraka wa Israel na Marekani na imeapa kuendelea kushikilia madaraka.

Lakini Jumuiya ya kimataifa imeikaribisha serikali hiyo mpya na inatarajiwa sana kuiondolea vikwazo vya kiuchumi na kidiplomasia vya miezi 15 vilivyokuwa na athari kubwa ambavyo viliwekwa baada ya Hamas linalohesabiwa kuwa kundi la kigaidi na Israel na mataiafa ya magharibi kuingia madarakani katika uchaguzi wa fadhaa hapo mwezi wa Januari mwaka 2006.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Havier Solana amesema kutakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na serikali hiyo kadhalika ule wa kiuchumi.

Rais George W. Bush wa Marekani leo hii pia amemuhakikishia kummunga mkono Abbas katika mazungunzo ya simu.

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert ambaye yuko nchini Marekani pia amedokeza kwamba nchi yake iko tayari kuitambuwa serikali hiyo mpya na kushirikiana nayo.

Amesema wataziachilia fedha ambazo walikuwa wakizishikilia chini ya udhibiti wao kwa sababu walikuwa hawataki fedha hizo zichukuliwe na Hamas ili kwamba wazitumie kama sehemu ya shughuli zao za kigaidi.

Wakati Rais Abbas akisisitiza kwamba matumizi ya serikali yake yatakuwa kwa maeneo yote ya Wapalestina bado haiko wazi vipi itaweza kuweka mamlaka yake kwa eneo la Gaza linalodhibitiwa na Hamas ambapo watu milioni 1 na nusu wanaishi wengi wao wakiwa katika hali mbaya.