1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali, waasi Sudan Kusini wasaini makubaliano

24 Januari 2014

Serikali na waasi wa Sudan Kusini wamesaini makubaliano ya kusitisha mapigano, lakini wachambuzi wanaona kwamba bado kuna kazi kubwa ya kuwadhibiti wapiganaji na kuufanya mkataba huo ufanye kazi.

https://p.dw.com/p/1AwVG
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia na mwenyekiti wa IGAD, Tedros Adhanom (katikati), kiongozi wa ujumbe wa serikali Nhial Deng Nhial (kushoto) na kiongozi wa ujumbe wa waasi Taban Deng (kulia) wakipeana mikono baada ya kusaini makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia na mwenyekiti wa IGAD, Tedros Adhanom (katikati), kiongozi wa ujumbe wa serikali Nhial Deng Nhial (kushoto) na kiongozi wa ujumbe wa waasi Taban Deng (kulia) wakipeana mikono baada ya kusaini makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.Picha: picture-alliance/dpa

Makubaliano hayo yaliyosainiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia, siku ya Alhamisi (tarehe 23 Januari 2014), yalitazamiwa kutekelezwa masaa 24 baasa ya kusainiwa kwake na hivyo kumaliza wiki tano za mapigano makali ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Mkuu wa ujumbe wa waasi kwenye mazungumzo hayo, Taban Deng, ameyaita makubaliano hayo kuwa ni chachu "itakayoandaa mazingira ya mdahalo wa kisiasa na ambao utafungua njia ya amani ya kudumu."

Mkuu wa ujumbe wa serikali, Nhial Deng Nhial, alisema mazungumzo hayo yaliyokuwa yakisuasua kwenye hoteli moja ya kifahari mjini Addis Ababa hayakuwa rahisi.

"Tunatarajia kuwa tutaweza kupiga hatua kuelekea makubaliano kamili ambayo yatamaliza umwagaji damu," alisema Nhial, lakini akaonesha wasiwasi wake juu ya uwezo wa waasi, ambao miongoni mwao ni vikosi vya kijeshi, wanamgambo wa kikabila na watu wa kawaida, kuweza kusimamisha ghasia.

Jumuiya ya kimataifa yawapongeza

Hatua ya wawakilishi wa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na wale wa hasimu na makamu wake wa zamani, Riek Machar, kuweka saini zao kwenye hati hiyo ilipokewa fursa na wapatanishi, wanadiplomasia na jumuiya ya kimataifa.

Wanajeshi wa serikali wakiingia kwenye mji wa Bor tarehe 18 Januari 2014.
Wanajeshi wa serikali wakiingia kwenye mji wa Bor tarehe 18 Januari 2014.Picha: Getty Images/AFP/Charles Lomodon

Rais Barack Obama wa Marekani, ambaye nchi yake iliwahi kuunga mkono kwa hali na mali juhudi za Sudan Kusini kuwa huru, ameyaelezea makubaliano hayo kama "hatua muhimu ya kwanza kuelekea utafutaji wa amani ya kudumu."

Rais Obama alisisitiza kwamba "Viongozi wa Sudan Kusini wanapaswa kuyatekeleza kikamilifu na haraka makubaliano hayo na kuanza mdahalo wa kisiasa unaowajumuisha wote ili kutatua chanzo cha mgogoro."

Vipengele vya Makubaliano

Wapatanishi kutoka Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki na Pembe ya Afrika (IGAD) walisema makubaliano hayo yataweka chombo cha usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezwaji na kuwaruhusu wafanyakazi wa misaada kufanya kazi zao kwa uhuru.

Wakimbizi wa Sudan Kusini wakisubiri kwenye mpaka wa Joda karibu na Sudan wakikimbia mapigano.
Wakimbizi wa Sudan Kusini wakisubiri kwenye mpaka wa Joda karibu na Sudan wakikimbia mapigano.Picha: Reuters

Vile vile, serikali ya Sudan Kusini imekubali kuwaachia wanasiasa 11, washirika wa Machar, ambao waliwekwa kizuizini baada ya mapigano kati ya makundi hasimu ya wanajeshi kuanza siku ya tarehe 15 Disemba, ingawa hakukutolewa tarehe rasmi ya kuachiwa kwao.

Suala la mahabusu hao ilikuwa mada iliyoleta mkwamo kwenye mazungumzo hayo na Obama alisisitiza kwamba ushirikia wao ungelikuwa "muhimu" sana kwenye utafutaji wa makubaliano katika siku zijazo.

Athari za mapigano

Katika wiki tano za mapigano haya, wachambuzi na wafanyakazi wa misaada wanaamini kwamba zaidi ya watu 10,000 wameuawa na wamezilaumu pande zote mbili za mzozo huo kwa kuhusika na utesaji na mauaji ya makusudi.

Wakimbizi wa Sudan Kusini kwenye kambi ya Tzaipi.
Wakimbizi wa Sudan Kusini kwenye kambi ya Tzaipi.Picha: Reuters

Zaidi ya watu 500,000 wamelazimika kuyahama makaazi yao wakati wa wimbi la ghasia za kikabila kwenye taifa hilo jipya na fukara.

Baada ya mapigano ya awali kuzuka kwenye mji mkuu Juba zaidi ya mwezi mmoja uliopita, mgogoro ulisambaa haraka na kuwa vita kamili kati ya jeshi lililoungwa na wanajeshi wa Uganda na wanajeshi walioasi wakishirikiana na makundi ya wanamgambo.

Ghasia hizo zilichukua sura ya kikabila pale watu wa jamii ya Dinka, ambalo ni kabila la Kiir, walipopambana na jamii ya Nuer, kabila la Machar, hali iliyopelekea maelfu kusaka hifadhi kwenye vituo vya walinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini humo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman