1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Serikali Afrika Kusini yakosolewa vifo mgodini vikifika 60

15 Januari 2025

Miili 60 na manusura 132 wametolewa mgodini, huku mamia wengine wakiwa bado wamekwama chini ya ardhi na juhudi za uokoaji zikiendelea. Serikali imeelezea uchimbaji haramu wa madini kama "vita dhidi ya uchumi,"

https://p.dw.com/p/4pAKR
Afrika Kusini | Uondoaji wa wachimbaji haramu katika mgodi wa dhahabu uliokuwa umefungwa huko Stilfontein
Wachimbaji haramu wakisindikizwa na maafisa wa polisi baada ya kuokolewa kutoka mgodi wa dhahabu ulioachwa bila kutumika kwa miezi kadhaa, Stilfontein, Afrika Kusini, Jumanne, Januari 14, 2025.Picha: Themba Hadebe/AP Photo/picture alliance

Serikali ya Afrika Kusini inakabiliwa na ukosoaji mkubwa kufuatia vifo vya wachimbaji haramu wasiopungua 60waliokwama chini ya ardhi kwa miezi kadhaa, baada ya polisi kuzingira mgodi kwa lengo la kuwakamata mara watakapojitokeza.

Shughuli ya uokoaji iliyoamriwa na mahakama ilianza Jumatatu, ambapo miili ya wachimbaji waliokufa na manusura 132 waliodhoofika sana walitolewa kutoka mgodini, huku mamia ya wengine wakiripotiwa kubaki umbali wa kilomita 2 chini ya ardhi kwenye mgodi wa dhahabu huko Stilfontein, kilomita 150 kutoka Johannesburg.

Polisi walizuia usambazaji wa chakula na maji kwa wachimbaji hao tangu Agosti, hadi mahakama iliporuhusu misaada ya dharura kupelekwa kwao mnamo Desemba.

Afrika Kusini | Uondoaji wa wachimbaji katika mgodi wa dhahabu uliositishwa shughuli zake huko Stilfontein
Familia za wachimbaji na wanaharakati wakifanya maandamano wakati Waziri wa Polisi wa Afrika Kusini, Senzo Mchunu, alipotembelea mgodi huo ulioko Stilfontein, Afrika Kusini, Jumanne, Januari 14, 2025.Picha: Themba Hadebe/AP Photo/picture alliance

Wachimbaji waliopatikana hai walikamatwa mara moja na kushtakiwa kwa makosa kama uhamiaji haramu, kuvamia mali, na uchimbaji haramu wa madini. Wachimbaji wengi walikuwa raia kutoka Msumbiji, Zimbabwe, na Lesotho, huku idadi ndogo wakiwa ni Waafrika Kusini.

Soma pia: Watu kadhaa waokolewa, miili yatolewa shimo la mgodi Afrika Kusini

Serikali ilitetea hatua yake, ikisema operesheni hiyo ilikuwa muhimu ili kudhibiti uchimbaji haramu unaosababisha hasara kubwa ya kifedha kwa taifa na sekta ya madini.

Hata hivyo, chama cha upinzani cha DA kiliitaka serikali kuunda tume huru kuchunguza tukio hilo na kuwawajibisha waliohusika, kikieleza kuwa hali hiyo imezidi kuwa mbaya na polisi walionyesha uzembe mkubwa.

Wakati huo huo, juhudi za uokoaji zinaendelea, zikitumia chombo maalum cha chuma kushusha na kuleta juu manusura pamoja na miili ya wachimbaji waliopoteza maisha.

Afrika Kusini | Oparesheni ya kuwaondoa wachimbaji katika mgodi wa dhahabu uliotelekezwa huko Stilfontein
Wahudumu wa idara ya uchunguzi wa jinai wakibeba mabaki ya miili katika mifuko ya rangi ya bluu wakati wa operesheni ya uokoaji wa wachimbaji kutoka chini ya ardhi katika mgodi wa dhahabu uliotelekezwa huko Stilfontein, Afrika Kusini, Jumanne, Januari 14, 2025.Picha: Themba Hadebe/AP Photo/picture alliance

Soma pia: Afrika 2025: Mapambano ya demokrasia na ukuaji

Wachimbaji haramu, wanaojulikana kama "zama zamas", mara nyingi huingia kwenye migodi iliyofungwa wakitafuta mabaki ya madini huku wengine wakiongozwa na magenge ya kihalifu yanayojihusisha na uchimbaji haramu.

Chama cha DA kiliongeza kuwa, licha ya uhalifu unaoambatana na uchimbaji haramu, wachimbaji wa kiwango cha chini mara nyingi ni watu waliokatishwa tamaa wanaojitahidi kutafuta riziki katika mazingira magumu.