Serikali ya Burundi: Nkurunziza hakufa kutokana na corona
10 Juni 2020Msemaji wa serikali ya Burundi ameiambia DW kwamba rais huyo amekufa kutokana na maradhi ya moyo. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari kadhaa kiongozi huyo alipelekwa hospitali ya jimbo la Karuzi mwishoni mwa wiki liyopita.
Kwanza alipata afueni lakini hapo Jumatatu hali yake iligeuka na kuzidi kuwa mbaya. Nkurunziza alikufa akiwa na umri wa miaka 55. Mke wake alipelekwa Kenya jumatatu hiyo hiyo kwa ajili ya matibabu ya corona.
Nkurunziza amekufa wakati rais mtuele Evariste Ndayishimiye anatarajiwa kuapishwa rasmi kushika madaraka wiki chache zizajo. Ndayishimiye alishinda uchaguzi wa rais nchini Burundi mwezi uliopita baada ya Nkurunziza kuamua kutogombea muhula mwingine.
Kifo cha Nkurunziza chaitikisa Burundi
Kifo chake ni kama tetemeko la ardhi nchini Burundi baada ya kuitawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 15. Wachambuzi wanasema sasa Burundi haiwezi tena kuficha ukweli juu ya janga la corona baada ya kifo cha kiongozi huyo na baada ya mke wake kupelekwa Nairobi kwa ajili ya matibabu ya maradhi hayo!
Burundi yatangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa
Hapo awali wachambuzi walitarajia kumwona Nkurunziza akivuta hatamu za uongozi nyuma ya kiongozi mpya Ndayishimiye. Mtaalamu wa masuala ya Burundi Thierry Vircoulon amesema huenda kifo cha Nkurunziza kimetokana na mkakati wa kisiasa.
" Rais mpya anaetokea kwenye utawala wa zamani sasa atakuwa na uwanja huru!" Amesema Thierry Vircoulon.
Wasifu wa Nkurunziza
Nkurunziza aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu nchini Burundi alikuwa kiongozi wa waasi katika miaka ya nyuma. Mnamo mwaka 2015 aligombea muhula wa tatu wa rais na miaka mitatu baadae alibadilisha katiba ya Burundi kwa njia ya kura ya maoni ambayo ingemwezesha kutawala hadi mwaka 2034.
Tangu aingie madarakani watu zaidi ya 400,000 waliikimbia Burundi na maelfu wameuawa. Mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague inafanya uchunguzi juu ya kukiukwa haki za binadamu wakati wa utawala wa Nkurunziza.