1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Lebanon yajiuzulu

11 Agosti 2020

Waziri mkuu wa Lebanon Hassan Diab ametangaza kujiuzulu kufuatia mripuko wa wiki iliyopita mjini Beirut na kusababisha madhara makubwa kuanzia makazi ya watu, vifo na hata majeruhi.

https://p.dw.com/p/3glZY
Libanon Beirut Premierminister Hassan Diab
Picha: Reuters/M. Azakir

Kwenye taarifa yake fupi kupitia televisheni, waziri mkuu Diab alisema anachukua hatua hiyo ili aungane na watu wa Lebanon na kwa pamoja wapiganie mabadiliko. Alinukuliwa akisema " Ninatangaza leo kujiuzulu kwa serikali hii. Mungu ailinde Lebanon"

Rais Michel Aoun amekubaliana na hatua hiyo ya serikali kujiuzulu.

Wiki iliyopita Diab alimlaumu mtangulizi wake kwa mripuko huo. Alisema wanasiasa wanatakiwa kuona aibu kwa sababu ufisadi ndio umesababisha janga hilo lililofichwa kwa miaka saba.

Alisema "ufisadi ndio chanzo cha janga hili. "Kile kilichopo katikati yetu na mabadiliko ni ukuta mwembamba unaolindwa na mbinu chafu"

Baadhi ya mawaziri tayari walikuwa wamejiuzulu hapo kabla, kufuatia maandamano makubwa ya kuipinga serikali yaliyoibuka baada ya mripuko huo kutokea.

Siku ya Jumatatu, waziri wa afya Hamad Hassan aliwaambia waandishi wa habari kwamba Diab alikuwa anaelekea kwa rais kumkabidhi barua ya kujiuzulu kwa niaba ya mawaziri wote, hatua iliyotanguliwa na kikao cha baraza la mawaziri.