1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Pakistan yapoteza uwingi bungeni

4 Januari 2011

Serikali ya Pakistan inayoongozwa na Waziri Mkuu Yousuf Raza Gilani imepoteza wingi wake bungeni, baada ya chama cha Muttahida Qaumi Movement-MQM- kujitoa katika serikali ya muungano, mwishoni mwa wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/QmbK
PM Yousaf Raza Gillani Foto Abdul Sabooh Januar 2010
Waziri Mkuu wa Pakistan, Yousuf Raza Gilani.Picha: Abdul Sabooh

Uamuzi wa chama cha MQM umekuja wakati ambapo serikali ya waziri mkuu Gilani inakabiliwa na uchumi ulioporomoka vibaya, huku ikishinikizwa na Marekani kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya wanamgambo. Kwa mujibu wa Christian Wagner, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na Asia ya Kusini, chama cha MQM tangu wiki kadhaa zilizopita, kilianza kujiweka mbali na serikali ya Gilani. Mvutano wa kwanza kati ya chama hicho na chama tawala cha PPP ulizuka katikati ya mwezi wa Desemba, pale waziri wa ndani katika jimbo la Sindh alipokituhumu chama cha MQM kuhusika na mauaji ya mpangilio katika eneo la Karachi.Amesema:

" Mzozo huo uliibuka tangu wiki kadhaa. Ninaamini kuwa hatua ya serikali kupandisha bei ya mafuta ya petroli, imetumiwa kuwa sababu ya kujitoa katika serikali hiyo ya mseto."

Wakati huo huo,Faisal Subzwari mwanasiasa mashuhuri wa MQM amesema,serikali inakabiliwa na vitisho mbali mbali. Bila shaka kuna matatizo ya uchumi na usalama wa ndani lakini changamoto kubwa kabisa ni uongozi bora wa serikali.

Kufuatia maafa yaliyosababishwa na mafuriko mwaka jana, serikali imepoteza sana umaarufu wake kwa kutochukua hatua za kutosha. Kwa hivyo,si ajabu kuona vyama vingi vikijaribu kujiweka mbali na serikali.

Nawaz Sharif the former Prime Minister and leader of opposition Pakistan Muslim League-Nawaz (PML-N) waves to supporters as he arrives at Allama Iqbal International Airport in Lahore, Pakistan, 25 November 2007. Nawaz Sharif returned to his homeland from Saudi Arabia today after seven years of exile, receiving an exuberant welcome from supporters of his PML-N opposition party. Pakistan President general Pervez Musharraf allowed Nawaz and his brother Shahbaz to return to Pakistan and contest upcoming parliamentary elections scheduled for January 2008.
Nawaz Sharif, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani PML-N.Picha: picture-alliance/ dpa

Lakini kundi kubwa kabisa la upinzani nchini humo halitoshinikiza kupigwa kura ya kutokuwa na imani dhidi ya Waziri Mkuu Gilani. Kwa maoni ya chama hicho cha PML-N kinachoongozwa na waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif, kura hiyo itaiathiri nchi nzima. Uamuzi huo humaanisha kuwa serikali inayoongozwa na chama cha Gilani cha PPP, huenda ikanusurika licha ya mshirika wake mkuu kujitoa serikalini siku ya Jumapili na hivyo kuinyima uwingi bungeni. Kwa upande mwingine, itakuwa vigumu sana kwa serikali hiyo kuimarisha uchumi, kupunguza umasikini na kupiga vita ugaidi bila ya kuungwa mkono na vyama vingine.

Mvutano huo wa kisiasa umeibuka wakati ambapo Pakistan inazidi kushinikizwa na Marekani kuyasaka makundi ya wanamgambo wa Kiislamu, ili kusaidia kubadili mkondo wa vita nchini Afghanistan.

Mwandishi: Bärthlein,Thomas/ZPR

Mpitiaji: Josephat Charo