Serikali ya Sudan Kusini kurefusha kipindi cha urais
4 Julai 2018Kulingana na wabunge wa Sudan Kusini waliozungumza na shirika la habari la Reuters, mswaada huo utalazimisha marekebisho ya katiba ili kuongeza muhula wa Rais Kiir hadi mwaka 2021.
Mbunge Paul Yoane Bonju amesema mswaada huo uliwasilishwa bungeni hapo jana Jumatatu na kwamba wabunge wanatarajiwa kuupitisha kuwa sheria mwezi huu wa Julai.
Aidha msemaji wa kundi la waasi la Riek Machar, Lam Paul Gabriel, amesema serikali inapendekeza hatua ambayo ni kinyume cha sheria ya kujaribu kuongeza muhula wa Rais Kiir madarakani.
Wiki iliyopita, Kiir na Machar walikutana na kutia saini makubaliano mapya ya amani yaliyojumuisha kusitisha mapigano, makubaliano ambayo yalitakiwa kuanza kutekelezwa siku ya Jumamosi.
Hata hivyo, makubaliano hayo yalivunjwa siku hiyo hiyo baada ya vikosi vya serikali na waasi kuanza kushambuliana.
Mapigano zaidi yashuhudiwa katika eneo la Upper Nile
Hapo jana, kulishuhudiwa mapigano zaidi katika eneo la Upper Nile yaliyosababisha mauaji ya watu 18. Taifa hilo changa duniani lililojipatia uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011, lilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwaka 2013 kufuatia mzozo kati ya Rais Kiir na makamu wa rais wa zamani, Riek Machar. Tangu wakati huo, maelfu ya watu wameuawa huku zaidi ya watu milioni tatu wakilazimika kuikimbia nchi hiyo.
Huku hayo yakiarifiwa, katika mkutano wa kilele wa Viongozi wa Umoja wa Afrika uliomalizika hapo jana nchini Mauritania, Mkuu wa Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, siku ya Jumaosi alitoa wito wa uwepo wa hatua fulani dhidi ya wahusika katika mgogoro wa Sudan Kusini akisema kwamba kwa sasa imezoeleka kwa wahusika hao kutoheshimu makubaliano wanayofikia. Mahamat amesema hali Sudan Kusini ni ya kutisha huku akisisitiza kwamba hali ya kibinaadamu na kiusalama inazidi kuwa ngumu kila kukicha.
Kwa upande wake, Umoja wa Mataifa ulitoa onyo kwa pande zote husika katika mgogoro wa Sudan Kusini kufikia makubaliano ya kisiasa mwishoni mwa mwezi Juni au wakabiliwe na vikwazo.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/dpa/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef