1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali,Waasi washutumiana kutofika misaada ya kiutu Tigray

Hawa Bihoga
30 Machi 2022

Serikali ya Ethiopia na waasi wa Tigray wameshutumiana kwa kuzuia msafara wa misaada ya kiutu uliokuwa na mahitaji ya dharura kwa wakaazi wanaokabiliwa na njaa katika eneo la kaskazini.

https://p.dw.com/p/49EVZ
Äthiopien | Premierminister nimmt an Offensive gegen Rebellentruppen Teil
Picha: Ethiopian Prime Minister's Office//AA/picture alliance

 

Serikali ya Ethiopia imewashutumu waasi kwa kuzuia misaada huku waasi wa TPLF wakisema hakuna misaada yoyote ya kiutu iliyowasili katika eneo la Tigray lililo na wakaazi takriban milioni sita wanaokabiliwa na hali mbaya ya kiutu.

Mnamo Machi 24 serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed ilitangaza kile ilichokiita makubaliano ya kibinaadamu ya muda mrefu yatakayoanza mara moja ili kurahisisha utoaji wa misaada ya dharura katika mkoa wa Tigray ambapo mamia kwa maelfu ya watu wanakabiliwa na njaa.

Soma zaidi:Serikali ya Ethiopia yatuhumu waasi kuzuia misaada

Saa kadhaa baadae waasi walikubali kusisitishwa kwa mapigano, ikiwa ni hatua mpya ya kuleta mabadiliko chanya katika vita vilivyodumu kwa takriban miezi 17 huko kaskazini mwa Ethiopia na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha.

Waasi: serikali ya Abiy itimize ahadi zake

Katika kile walichokiita makubaliano kila upande ulitoa masharti, serikali ikitoa wito kwa chama cha Ukombozi wa watu wa Tigray TPLF kuachana na vitendo vyote vya uchokozi na kujiondoa katika maeneo ya mikoa ya jirani ambayo imeyamiliki ya Afar na Amhara.

Kwa upande wa waasi wamezitaka mamlaka za Ethiopia kutokutoa ahadi hewa badala yake wachukue hatua madhubuti ili kuwezesha ufiakiaji wa misaada ya kiutu usio na vikwazo kwa Tigray.

Äthiopien Amhara | Militär auf der Straße
Askari wa ulinzi wa jeshi la Ethiopia katika mitaa ya mji wa AmharaPicha: Minasse Wondimu Hailu/Anadolu Agency/picture alliance

Tangu kuafikiwa kwa makubaliano hakuna lori lolote la misaada ya kiutu, ambayo yapo katika eneo la Semera katika mji mkuu wa Afar tangu Decemba 15 yakisubiri kupeleka misaada ya dharura huko eneo la Tigray.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne, serikali ilisema kwamba imekuwaikitumia njia zote zilizopo kuwaokoa raia  katika eneo la Tigray lakini haijaweza kupata ushirikiano wa upande wa waasi.

soma zaidi:UN: Zaidi ya watu 300 wameuawa Ethiopia tangu Novemba

Msafara wa malori 43 ya msaada wa chakula, zilitolewa na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP hazijaweza kuwasilishwa katika eneo la Tigray kutokana na kufungwa kwa Barabara ya Abala na wanamgambo wa TPLF. Ilisema sehemu taarifa hiyo iliotolewa na serikali.

Taarifa walioitoa hapo jana waasi wa TPLF walisema kwamba hakuna msaada wa kibinadamu ambao umefika Tigray, huku wakilaani kile walichokiita madai ya uwongo ya mamlaka ya Ethiopia kwamba waasi hao wanazuia misaada, na kutaka uwasilishwaji wa misaada ya kiutu usio na kikwazo  utenganishwe na masuala ya kisiasa.

UN:Wakaazi Tigray wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula

Shirika  la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa mwezi Januari lilikadiria kuwa watu milioni 4.6  kati ya milioni 6 huko Tigray hawana uhakika wa chakula  huku milioni mbili wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Welternährungsprogramm der Vereinten Nationen
Ndege ya WFP ikishusha msaada wa chakulaPicha: Maciej Moskwa/NurPhoto/picture-alliance

Tangu mwezi Februari  utolewaji wa misaada ya kibinadamu huko Tigray ambapo zaidi ya watu 400.000 wameyakimbia makazi yao kutokana na mzozo huo umesitishwa kulingana na Umoja wa mataifa.

Soma zaidi:Ethiopia: Wapiganaji wa Tigray walaumiwa kwa ubakaji

Mzozo huo ulianza wakati waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alipotuma wanajeshi huko Tigray kuiangusha TPLF, chama tawala cha zamani cha eneo hilo, akisema hatua hiyo ilikuja kujibu mashambulizi ya waasi kwenye kambi za jeshi.

 Mapigano yameendelea, na kusababisha mzozo wa kibinadamu, huku pande zote zikishutumiwa kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Chanzo:AFP