Presseschau
6 Februari 2008Matangazo
Bado haijulikani kitu gani kilichosababisha kutokea moto katika mji wa Ludwigshafen hapa nchini Ujerumani na ambao uliwaua watu tisa. Kwa vile hasa waliokuwa ni familia yenye asili ya kituruki iliyokuwa ikiishi katika nyumba iliyoathirika, tukio hili lilisababisha pia hasira kubwa nchini Uturuki. Ndiyo sababu, waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan anaitaka Ujerumani ichunguze kwa kina ikiwa nyumba ilichomwa ni kitendo cha uhalifu dhidi ya wageni au kama ilikuwa ajali tu. Uturuki pia imetuma maafisa ambao wanajiunga na polisi wa Ujerumani kupeleleza jambo hilo. Kutokana na haya wahariri wengi leo hii wanaangalia mahusiano kati ya Wajerumani na Waturuki kama mwandishi huyu wa gazeti la "Tageszeitung" la mjini Berlin:
"Bado huwezi kufutilia mbali uwezekano wa kitendo cha uhalifu dhidi ya wageni. Mtoto mmoja alisema alimwona mwanamume aliyeongea Kijeruamani ambaye aliwasha moto. Lakini hakuna mengine yanayojulikana hadi sasa. Hata hivyo, vyombo vya habari vya Uturuki vinakisia juu ya chanzo cha moto huu na ulikuwa na vichwa vya habari. Gazeti moja hata limeandika ni vita. Hii ni ishara kwamba mahusiano kati ya Wajerumani na Waturuki ni ya kutoaminiana."
Na katika gazeti la "Tagesspiegel" ambalo pia linachapishwa mjini Berlin tunasoma hivi:
"Wote waliouawa ni wa asili ya Kituruki na tena mashambulio ya kuchomwa moto nyumba za wageni yameshawahi kutokea mara kadhaa hapa nchini. Kwa hivyo ni hatua ya busara kwamba serikali ya Ujerumani imekubali ombi la waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan, na kuwahusisha maafisa wa Uturuki katika uchunguzi unaoendelea. Lengo ni kuweka wazi kabisa yanayojulikana. Bila shaka, wote ikiwa ni Wajerumani au Waturuki wanatumai kuwa chanzo si shambulio la kihalifu."
Suala jingine linalozusha mjadala mkubwa ni kisa cha matumizi mabaya ya fedha katika tawi la Ujerumani la shirika la kimataifa la kuwasaidia watoto UNICEF. Kulingana na uchunguzi wa hivi karibuni, tawi hili limelipa fedha nyingi mno kwa washauri. Mhariri wa "Nordsee-Zeitung" ameandika hivi:
"Kweli, ni kashfa kubwa. Mamillioni ya watoto duniani kote wanategemea msaada kutoka kwa UNICEF na michango ya watu binafsi. Hata hivyo, shirika hilo haliwezi kutoa mwanga katika tuhuma za kutumia vibaya fedha. Tayari, michango imepungua kwa kiasi kikubwa. Ikiwa tuhumu hizo ni kweli, inabidi watu husika wajiuzulu."
Na hatimaye haya hapa ni maoni ya gazeti la "Augsburger Allgemeine" kuhusu kashfa ya UNICEF:
"Shirika la UNICEF limepoteza uaminifu wake wote ambao ni mali muhimu zaidi ya shirika lolote la kutoa misaada. Jambo baya zaidi lakini ni kwamba shirika la UNICEF limeharibu uaminifu wa sekta nzima ya misaada, pia mashirika ambayo yametumia vizuri michango ya watu binafsi."
Matangazo