1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio dhidi ya ubalozi mdogo wa Marekani huko Pakistan

5 Aprili 2010

Waislamu wenye siasa waliushambulia ubalozi mdogo wa Marekani leo katika mji wa Peshawar, Pakistan,

https://p.dw.com/p/MneV
Shambulio la leo la kigaidi katika ubalozi mdogo wa Marekani mjini Peshawar, PakistanPicha: Faridullah Khan

Waislamu wenye siasa kali, wakiwa na bunduki, makombora na mabomu yanayotegwa katika magari na watu wenye kujitoa mhanga waliushambulia ubalozi mdogo wa Marekani hii leo katika mji wa Peshawar, kaskazini magharibi ya Pakistan, na pia kuushambulia mkutano wa hadhara, hivyo kuwauwa jumla ya watu 46. Mashambulio  hayo yaliotokea moja baada ya jengine, ndio yalio mabaya kabisa mnamo mwaka huu katika Pakistan ambako hali ya kukosekana usalama imezidisha wasiwasi huko Marekani juu ya namna vita vinavoendelea huko Afgahnistan na pia vile dhidi ya mtandao wa kigaidi wa al-Qaida.

Zaidi anayo Othman Miraji...

Wataliban wa Pakistan wamedai kwamba wao ndio waliushambulia ubalozi mdogo wa Marekani mjini Peshawar, wakidai ilikuwa ni kulipiza kisasi kwa mashambulio yanayofanywa na ndege za Marekani zikizokuwa na rubani, zikiwalenga viongozi wa  wapiganaji wa Kitaliban katika maeneo ya mpaka baina ya Pakistan na Afghanistan. Taarifa ya leo ya Wataliban ilitishia kufanywa mashambulio zaidi dhidi ya Wamarekani.

Uwezo wa wapiganaji hao waliokuwa na silaha nzito kuukaribia ubalozi mdogo wa Marekani pamoja na vituo vingine vya kijeshi, kama vile makao makuu ya kimkoa ya wakala wa ujasusi wa waziri mkuu wa Pakistan, huenda sana yakazitia wasiwasi serekali za Marekani na Pakistan.

Si chini ya wapiganaji sita wa Kitaliban, wakiwa na baruti na gari mbili zilizokuwa na mabomu, waliulenga ubalozi huo mdogo unaolindwa vikali  na ulioko katika mji wa Peshawar ulio na wakaazi milioni 2.5, hivyo kusababisha miripuko kadhaa.

Marekani ilililaani shambulio hilo la kigaidi, ikisema si chini ya walinzi wa usalama wawili wa Kipakistan walioajiriwa na ubalozi huo mdogo waliuwawa na idadi ya wengine walijeruhiwa vibaya. Ubalozi wa Marekani mjini Ilslamabad ulisema shambulio hilo lililoowanishwa liliihusisha gari iliokuwa na mabomu ya watu wenye kujitoa mhanga pamoja na magaidi waliojaribu kuingia katika jengo hilo la ubalozi mdogo, wakitumia makombora na bunduki. Polisi ilisema magari mawili yaliokuwa na mabomu yaliripuka katika  kizuizi cha kugaua watu, mita 50 kutoka jengo hilo, na gari jengine lilokuwa na kilo mia moja za baruti karibu na lango la ubalozi huo mdogo, kukifuata  moto mkubwa.

Waziriwa habari wa mkoa wa kaskazini magharibi ya Pakistan, Mian Iftikhar Hussain, aliwaambia waandishi wa habari kwamba maafisa watano wa usalama na wapiganaji sita waliuwawa, akilinganisha na hujuma iliofanywa mwezi Oktoba mwaka jana katika  makao makuu ya kijeshi ya Pakistan. Aliwaambia waandishi wa habari katika hospitali kuu ya mji wa Peshawar kwamba magaidi walitumia mbinu zilezile na mtindo ule ule walioutumia walipoyashambulia makao makuu ya jeshi; walikuwa na magari, maroketi na walikuwa na watu wa kujiripuwa. Kizuizi cha usalama karibu na lango la ubalozi huo mdogo kiliharibiwa, na makombora yaliwachiwa ardhini katika eneo hilo ambalo lilizingirwa na polisi pamoja na jeshi la Pakistan.

Waziri mkuuwa Pakistan, Yousuf Raza Gilani, alisema watu hao waovu walikuwa wanajaribu kusambaza hofu miongoni mwa watu katika jaribio lao la kutaka kuizorotesha operesheni ya serekali dhidi ya magaidi. Hisia dhidi ya Marekani zimeongezeka sana huko Pakistan, ambako  mashambulio ya maroketi ya Marekani ambayo yamewauwa zaidi ya watu 830 tangu Agosti mwaka 2008, na kuengezeka tangu Rais Barack Ovbama azidishe juhudi za kuvimaliza vita vya Afghanistan.

 Azam Tariq, msemaji wa Wataliban wa Pakistan, aliliambia  shirika la habari la Kifaransa, AFP, kw anjia ya simu kutoka mahapa pasipotajwa kwamba wao wamefanya mashambulio hayo dhidi ya ubalozi mdogo wa Marekani, na ni kulipiza kisasi kwa mashambulio yaliofanywa na ndege za Kimarekani zisizokuwa na marubani, na watafanya mashambulio zaidi ya aina hiyo na kulenga mahala popote walipo Wamarekani.

Leo pia mtu aliyejiripua kwa kujitoa mhanga aliushambulia mkutano wa hadhara katika wilaya ya Dir ambako Pakistan ilienedesha hujuma kubwa dhidi ya wapiganaji wa Kitaliban katika eneo hilo mwaka jana. Shambulio hilo liliwauwa watu 41 wakati wa sherehe zilizoandaliwa na chama kikuu cha kisiasa cha Awami National kisichoelemea dini na kinachotawala katika mkoa wa Kaskazini Magharibi. Sherehe hizo zilitokana na kukubaliwa mpango wa kupewa jina lengine mkoa wa  Kaskazini magharibi ya Pakistan, siku za mbele uitwe Khyber-Pakhtunkhwa. Jina hilo jipya linawapa heshima Wakaazi wa Ki-Pashtun walio wengi katika mkoa huo, na kuwa badala ya jina  lilokuwa linatumiwa tangu utawala wa kikoloni wa Kiengereza. Hiyo ni sehemu ya mpango wa kutoa mamlaka zaidi kwa mikoa.

Naye  mkuu wa siasa za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, ameyalaani mashambulio hayo ya leo nchini Pakistan na kulaumu vitendo hivyo vya utumiaji nguvu ambavyo vinajaribu kuizorotesha demokrasia nchini humo na katika eneo hilo.

Mwandishi:Othman Miraji /AFP

Mpitiaji:Abdul-Rahman