Shambulizi la droni lashambulia kinu cha nyuklia Ukraine
9 Aprili 2024Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki limesema mlipuko uliotokea mapema leo ukidaiwa kusababishwa na shambulizi la droni katika kinu kikubwa kabisa cha nyuklia barani Ulaya sio kitisho cha moja kwa moja katika usalama wa kinu hicho. Hata hivyo, shambulizi hilo limeonyesha hatari kubwa inayokikabili kinu hicho.
Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki limesema liliarifiwa kuwa mlipuko huo ulitokea mapema hii leo katika eneo la kituo cha mafunzo kilichopo karibu na kituo cha kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia.
Soma zaidi. Urusi: Ukraine imeshambulia kinu cha nyuklia Zaporizhzhia
Kituo cha Zaporizhzhia ni moja ya vinu 10 vikubwa vya nyuklia duniani. Mapigano yanayoendelea kusini mwa Ukraine yameibua hofu kwamba kuna uwezekano wa maafa ya nyuklia kama yale yaliyotokea Chernobyl mnamo 1986, ambapo kinu kililipuka na kusambaza miozi iliyoharibu eneo hilo.
Katika miezi ya hivi karibuni sio Urusi wala Ukraine amabyo imeweza kusoga mbele zaidi katika uwanja wa mapambano kwa walau kilomita 100 katika upande wa kusini mashariki ingawa mashambulizi ya droni na makombora yameendelea kuvurumishwa katika vita hivyo.
Soma zaidi. Zelensky aliomba bunge la Marekani kuidhinisha msaada wa nchi yake
Mara kwa mara Urusi na Ukraine zimekuwa zikitupiana lawama za mashtaka juu kinu cha Zaporizhzhia. Siku ya Jumatatu, Moscow ilidai kuwa Ukraine ilikuwa nyuma mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye kituo hicho siku moja kabla, na Kyiv kuishutumu Urusi kuwa inatumia mbinu hizo ili kupotosha.
Watu 300,000 wangehama makazi yao
Kwa mujibu wa shirika la kutoa huduma za dharura nchini Ukraine ni kwamba shambulio hilo lingeweza kusababisha maafa makubwa ambayo yangelazimu takriban watu 300,000 kuyahama makazi yao.
Soma zaidi.Ufaransa kujenga mahusiano yenye uwiano na Afrika
Wakati hayo yakiendelea, Rais wa Ukraine Vodymyr Zelensky amekagua ngome zake za kijeshi katika eneo la kaskazini mashariki la Kharkiv kutoa mwito wa kuomba msaada wa haraka wa kijeshi wakati Urusi ikizidisha mashambulizi yake ya anga katika eneo hilo.
Zelenskyy amekuwa akiyasisitiza mataifa ya magharibi kwamba waisaidiae nchi yake silaha zaidi ili iendeleze mapambano yake ya kujilinda dhidi ya uvamizi wa Urusi, katika maelezo yake ameiasa pia Marekani kupitisha muswada wa dola bilioni 60 ambao umeshikiliwa na bunge la Marekani tangu mwaka uliopita na kwamba kama Marekani isipotoa msaada huo Ukraine itapoteza vita dhidi ya Urusi.
Kwa upande mwingine, waziri wa mambon ya nje wa Uingereza David Cameron yuko ziarani nchini Marekani kuishinikiza kambi ya chama cha Republican kuruhusu pesa hizo ambazo zinapaswa kupelekwa nchini Ukraine baada ya kukutana na rais wa zamani Donald Trump.
Cameron amesema ushindi kwa Ukraine ni muhimu kwa usalama wa Marekani na Ulaya lakini rais huyo wa zamani na anayetarajiwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Republican ni mkosoaji wa msaada unaoendelea kutolewa na Marekani kwa Ukraine.