Sheikh Hasina ashinda tena Bangladesh
31 Desemba 2018Chama tawala cha Sheikh Hasina cha Awami League na washirika wake wameshinda viti 288 katika bunge lenye jumla ya viti 300, huku chama kikuu cha upinzani kikipata viti sita tu.
Hasina ambaye amepata muhula wa nne, amepinga madai ya upinzani kuhusiana na makabiliano kati ya wafuasi wa vyama hasimu ambayo yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 17 pamoja na madai ya wizi wa kura na vitisho.
"Uchaguzi ulikuwa huru na wa haki. Hakuna shaka juu ya hilo," alisema Hasina mwenye umri wa miaka 71. "Sina cha kuficha. Kila ninachokifanya nakifanya kwa ajili ya nchi. Dhamira yangu iko wazi kabisaa," aliongeza katika matamshi aliyoyatoa mbele ya waandishi wa habari.
Hasina amesisitiza hakuwa na tamaa ya "kusalia madarakani" na kwamba wapigakura waliunga mkono chama chake kwa sababu ya ukuaji wa kiuchumi nchini Bangladesh wakati wa uongozi wake wa muongo mmoja.
Muungano wa upinzani unaoongozwa na chama cha Bangladesh National Party (BNP) umesema umelengwa na katika ukandamizaji kwa miezi kadhaa kuelekea uchaguzi wa Jumapili na kutoa wito wa kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Miito ya uchaguzi mpya
"Tunataka uchaguzi mpya ufanyike chini ya serikali isioegemea upande mapema iwezekanavyo," kiongozi wa muungano wa upinzani Kamal Hossain aliwambia waandishi habari. Mamlaka ya uchaguzi imesema haijapokea malalamiko yoyote dhidi ya uchaguzi huo.
Hasina amesifiwa kwa kuimarisha ukuaji wa uchumi katika taifa hilo maskini la Asia Kusini na kwa kuwakaribisha wakimbizi wa Rohingya wanaokimbia ukandamizaji wa jeshi katika taifa jirani la Myanmar.
Lakini wakosoaji wanatuhumu utawala wake wa mkono wa chuma. Hasimu wake mkubwa na kiongozi wa chama cha BNP Khaleda Zia alifungwa kwa miaka 17 mwaka huu kwa mashtaka ya rushwa ambayo chama chake kinasema yalichochewa kisiasa.
Vurugu za umuagaji damu zimehanikiza kampeni za uchaguzi na kusambaa hadi siku ya uchaguzi, hata licha ya serikali kusambaza wanajeshi 600,000 nchini kote. Watu 13 waliuawa katika makabiliano kati ya wafuasi wa vyama vya Awami League na BNP, ilisema polisi.
Watu watatu walipigwa risasi na polisi waliosema walikuwa wanalinda vibanda vya kupigia kura. Askari polisi moja aliuawa pia na wanaharakati wa upinzani waliokuwa na silaha, kulingana na maafisa. Polisi sasa imethibitisha vifo 21 wakati wa kampeni na siku ya uchaguzi.
Salaam za pongezi zaanza kumiminika
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alikuwa kiongozi wa kwanza wa kimataifa kumpigia simu Hasina na kumpongeza, alisema katibu wa habari wa waziri mkuu huyo wa Bangladesh. Rais wa China Xi Jinping pia alimtumia salamu Hasina na kumpongeza kupitia ujumbe uliowasilishwa na balozi wa China nchini Bangladesh.
Wataalam wanasema ushindi wa Hasina utatiwa doa na tuhuma kwamba aliwaminya wapinzani. "Matokeo haya yanaathiri mfumo wetu wa demokrasia na huenda yakaharibu taasisi za kiserikali," Sakhawat Hussain, kamishna wa zamani wa uchaguzi aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP.
Upinzani unadai kuwa wanaharakati wake karibu 21, 000 waliwekwa kizuwizini wakati wa kampeni, na kuvunja uwezo wake wa kuhamasisha wapigakura.
Wagombea wake 35 walikamatwa kuhusiana na kile walichosema yalikuwa mashitaka ya kupangwa au kuondolewa katika kinyang'anyiro na mahakama, ambazo wapinzani wa Hasina wanasema zinadhibitiwana serikali.
Uongozi wa Bangladesh umekuwa ukizunguka kati ya Hasina na Zia, washirika waliogeuka kuwa madui, katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita. Ushindi wa Hasina umempatia muhula wake wa tatu mfululizo madarakani, na wa nne kwa ujumla.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Sekione Kitojo