Sherehe za ukombozi wa Bastille Ufaransa
14 Julai 2017Akijikuta anatengwa katika jukwaa la kimataifa, Donald Trump anaetajikana kuwa "rafiki wa Ufaransa amealikwa kama mgeni wa heshima kushiriki katika sherehe hizo zinazofanyika kila julai 14 katika Champs Elysée pamoja na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atakaeelekea baadae katika mji wa mwambao wa bahari ya Mediterenia, Nice, kuhudhuiria kumbukumbu za kuwaakumbuka wahanga 86 wa shambulio la kigaidi lililotokea mwaka mmoja uliopita.
Gwaride la kijeshi la mwaka huu linalofanyika wakati mmoja na kuadhimishwa miaka 100 tangu Marekani ilipoingia katika vita vikuu vya kwanza vya dunia, limefunguliwa na kikosi maalum cha wanajeshi wa Marekani "Sammies" waliovalia mavazi ya kijeshi ya wakati ule, wakifuatiwa na jumla ya wanajeshi 3720, magari 211 ya kijeshi, zikiwemo pikipiki 62, farasi 241 ndege za kivita 63 na helikopta 29.
Rais Trump asifu uhusiano wa Ufaransa na Marekani
"Ni sherehe kubwa na kuvutia ya taifa.Tuna pupa ya kushiriki. Sherehe ya aina peke'' alisema rais wa Marekani katika mkutano na waandishi habari pamoja na mwenyeji wake Emmanuel Macron katika kasri la Elysée.
"Mataifa yetu mawili yameungana, tuko pamoja milele , katika fikra ya kimapinduzi na kupigania uhuru" ameongeza kusema rais huyo wa Marekani.
Rais Emmanuel Macron atatoa hotuba fupi mwishoni mwa gwaride hilo kukumbusha umuhimu wa siku kuu hii ya taifa, iliyochanganyika hivi sasa na kumbukumbu za kuwakumbuka wahanga wa mashambulio ya kigaidi ya Nice-mashambulio yanayoihuzunisha Ufaransa kwa jumla.
Wafaransa wawakumbuka pia wahanga wa mashambulio ya Nice
Gwaride la mwaka huu linafanyika katika hali ya mvutano kati ya rais Macron na wanajeshi waliopaza sauti kulalamika dhidi ya hatua za kupunguzwa bajeti hatua ambazo zinalihusu pia jeshi la Ufaransa.
Gwaride la kijeshi katika uwanja wa Champs Elysée linatarajiwa kumalizika muda mfupi kutoka sasa.
Mara baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuondoka Paris kurejea Marekani, rais Macron atakwenda Nice kukutana na familia za wahanga wa shambulio la mwaka jana la kigaidi pamoja pia na watumishi wa idara za usalama na waokozi. Gwaride la kijeshi litafanyika pia Nice na kuonyeshwa moja kwa moja na vituo ya televisheni nchini humo. Mishumaa 86 imewashwa tangu leo asubuhi kabla ya rais Emmanuel Macron kuwasili, mishumaa inayokumbusha maisha ya watu 86 waliouliwa na gaidi mmoja aliyeendesha lori kati kati ya umati wa watu katika uwanja mashuhuri wa Promenade des Anglais.
Burudani itafanyika leo usiku kabla ya mabofu kurushwa hewani. Hakuna fashi fashi zitakazofyetuliwa lakini , wakaazi wa eneo hilo la kusini mashariki wanataka kushadidia msiba walio nao.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri:Gakuba, Daniel