1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo lamuelemea Zuma

3 Novemba 2016

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ameendelea kukutana na wakati mgumu baada ya kuongezeka kwa miito ya kumtaka kujiuzulu ambapo hivi sasa anakabiliwa na kura ya bunge kutokuwa na imani nae itakayofanyika wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/2S6e6
Südafrika Tausende protestieren vor Präsidentenpalast gegen Zuma
Picha: Reuters/M. Hutchings

 Maelfu ya raia wameandamana kwenye viunga vya mji wa Pretoria nchini Afrika Kusini kushinikiza Zuma kuachia madaraka.

Kura hiyo imeitishwa na chama kikuu cha upinzani alhamisi hii(03.11.2016) kufuatia ripoti ya taasisi ya kupambana na ufisadi nchini humo kutaka kufanyika kwa uchunguzi juu ya madai hayo yanayowagusa zaidi viongozi wa juu wa serikali kutoka chama tawala nchini humo, cha African National Congress, ANC. 

Kiongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani, cha Democratic Alliance, DA, Mmusi Maimane, amesema katika mkutano mfupi na waandishi wa habari mjini Cape Town kwamba majadiliano na kura ya kutokuwa na imani na rais Zuma yatafanyika wiki ijayo, Novemba 10.

Zuma mwenye umri wa miaka 74 amefanikiwa kuruka vihunzi viwili vya kura ya kutokuwa na imani naye katika kipindi cha mwaka huu, baada ya kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na wanachama wa chama chake cha ANC kinachohodi theluthi tatu ya viti vya bunge. Hata hivyo, afisa wa chama hicho ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wabunge wa ANC wanataraji kuachilia mbali kumuunga mkono Rais Zuma, na safari hii wataunga mkono hatua zitakazofikiwa. 

Jacob Zuma Korruption Prozess
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma anayekabiliwa na shinikizo la kuondoka madarakaniPicha: Getty Images/AFP/R. Jantilal

Tangu kuingia madarakani mwaka 2009, Rais Zuma amefanikiwa kushinda mlolongo wa kashfa nzito za ufisadi. Hata hivyo ripoti ya sasa ya taasisi hiyo ya kupambana na rushwa, maandamano ya raia na kura ya kutokuwa na imani nae kwa pamoja vinaongeza shinikizo kwa kiongozi huyo kuachia ngazi, kuliko wakati mwingine wowote. Na kama ataendelea kusalia madarakani, kuna wasiwasi wa  mahasimu wake walio ndani ya chama cha ANC kukabiliana nae.

"Mihemko ya raia nchini humo imeonyesha dhahiri kuwa imejawa na ghadhabu" imesema sehemu ya taarifa na kundi jipya linalojumuisha maveterani waliopambana na ubaguzi wa rangi, wanaharakati wa kiraia, wafanyabiashara na viongozi wa dini, linalojiita Save South Afrika. Miongoni mwa waratibu wa maandamano hayo, ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya madini ya Anglo-Gold Ashanti Sipho Pityana akasema.

Uchunguzi uliofanywa na ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali umeeleza kwa kina madai kwamba Zuma aliihakikishia familia ya Gupta kupata zabuni kupitia kampuni zinazomilikiwa na serikali na kuwa na uwezo wa kuchagua baraza la mawaziri. Naibu waziri wa fedha  Mcebisi Jonas aliwaambia wachunguzi kwamba Zuma alimpeleka nyumbani kwa Gupta, ambapo Gupta mwenyewe alimwambia kwamba atateuliwa kuwa waziri wa fedha.

Ripoti hiyo pia imeonyesha ushahidi wa simu kwamba David Van Rooney, mfuasi wa Zuma asiejulikana sana, alikuwa akiwasiliana  mara kwa mara na familia ya Gupta kabla ya uteuzi wake wa muda mfupi kuwa waziri wa fedha mwaka jana. Hata hivyo familia a Gupta amepinga tuhuma zote hizo na kutaka kufanyike uchunguzi.

Wakati hayo yakitokea, leo hii rais Jacob Zuma amesafiri kuelekea nchini Zimbabwe. Zuma ambaye ameambatana na nusu ya baraza la mawaziri amekutana na mwenyeji wake, Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe mjini Harare na kusaini makubaliano ya mashirikiano kati ya nchi hizo.

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Iddi Ssessanga.