Shinikizo laongezeka kwa May kujiuzulu
23 Mei 2019Hali hiyo inaondoa mtazamo kutoka uchaguzi wa Ulaya ambao hali itaonesha kwamba Uingereza bado inakabiliwa na mgawanyiko kuhusiana na suala la talaka kuachana na Umoja wa Ulaya.
Wakati kuna mkwamo mjini London, taifa hilo lenye uchumi mkubwa wa tano duniani linakabiliwa na tafakuri nyingi , ikiwa ni pamoja na kujitoa kwa utaratibu mzuri kwa kupata makubaliano, kujitoa bila makubaliano, uchaguzi ama kura ya pili ya maoni.
May, ambaye aliingia madarakani katika wadhifa huo wa juu kabisa katika kipindi cha mtafaruku ambacho kilifuatia kura ya maoni ya mwaka 2016 kuhusiana na uanachama wa Umoja wa Ulaya, ameshindwa mara kadhaa kulifanya bunge kuidhinisha makubaliano yake ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya ambayo amepigia upatu kuwa ni njia ya kuponya mgawanyiko uliopo wa Brexit nchini humo.
Kura ya pili ya maoni
Lakini katika juhudi zake za mwisho, akitoa uwezekano wa kuwa na kura ya pili ya maoni pamoja na utaratibu wa ukaribu wa kibiashara na Umoja wa Ulaya , zimezusha uasi kutoka kwa baadhi ya mawaziri wanaounga mkono Brexit. Kiongozi wa wabunge wa chama cha Conservative bungeni Andrea Leadsom amejiuzulu na huenda wengine zaidi wakafuatia.
Alipoulizwa kwanini anajiuzulu sasa Leadsom alisema.
"Kwa sababu nimekuwa nikiunga mkono Brexit kwa jumla kwa miaka mitatu iliyopita na siwezi tena, kama kiongozi wa baraza la wawakilishi nikiwa na jukumu la kibunge, nikisimama katika maswali na majibu kesho na kutangaza mswada ambao una vipengee ambavyo siwezi kuviunga mkono, ambavyo si vya Brexit."
"Siamini tena kwamba mtazamo wetu unaweza kufanikisha matokeo ya kura ya maoni," Leadsom , mmoja kati ya waliowania kiti cha waziri mkuu pamoja na May, alisema katika barua yake ya kujiuzulu.
May, ambaye ameonesha ushupavu katika kipindi ambacho kimekuwa na hali ngumu ya vurumai akiwa waziri mkuu katika historia ya hivi karibuni nchini Uingereza, ameahidi kuondoka madarakani iwapo wabunge wataidhinisha makubaliano yake ya Brexit lakini kwa sasa yuko katika shinikizo kubwa kutaaj tarehe ya kuondoka.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Josephat Charo