1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la WFP laonya kuhusu njaa Msumbiji

Daniel Gakuba
23 Septemba 2020

Mpango wa chakula duniani WPF umeonya kuwa maelfu ya wananchi wa Msumbiji wanakabiliwa na kitisho cha njaa.

https://p.dw.com/p/3isWl
Mosambik Children's Day in Inhambane
Picha: DW/L. da Conceicao

Hali hiyo imejiri baada ya raia kuyahama makaazi yao kuepuka ghasia zinazohusishwa na wanamgambo wenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Mashambulizi ya wanamgambo hao katika jimbo la Cabo Delgado lililo karibu na Tanzania yalianza mwaka 2017 lakini yameongezeka mwaka huu wa 2020, baada ya wanamgambo hao kuikamata miji muhimu kwa muda na kuvilenga shabaha vituo vya jeshi la serikali.

Katika ripoti yake mpya, WFP imesema watu 300,000 wameukimbia mkoa wa Cabo Delgado na kuhamia mikoa jirani, na baadhi yao wakivuka na kukimbilia Tanzania ambako hawafikiwi na msaada wa binadamu.

Shirika hilo limesema mzozo huo na kuhama kwa watu vitaongeza hatari ya maambukizi ya virusi vya corona. Hadi sasa Msumbiji imesajili visa 7,000 vya maambukizi ya COVID-19, na vifo 44 kutokana na maradhi hayo.