1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa za Kenya zachukua mkondo mpya kuelekea uchaguzi Mkuu

24 Januari 2022

Vyama vya Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi, United Democratic Alliance (UDA), cha makamu wa Rais William Ruto na kile cha Ford Kenya cha Moses Wetangula vimeamua kushirikiana kwenye uchaguzi mkuu ujao.

https://p.dw.com/p/45zz3
Niederlande Kenia Anhörung zu Gewalt nach Präsidentenwahl in den Haag William Samoei Ruto
Picha: AP

Akizungumza kwenye kongamano la Wajumbe la Taifa, la chama cha ANC, Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto amethibitisha kuwa vyama hivyo vitashirikiana kwa maslahi ya taifa.

Yaelekea kuwa mtetemeko wa ardhi ulioahidiwa na kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi umeyatikisa mawimbi ya siasa nchini Kenya. Muungano wa Kenya Moja ambao Musalia alikuwa mwanachama ukitangulia kuwa mwathiriwa baada ya tangazo lake.

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka na mwenzake wa Kanu Gideon Moi wametangaza kutalakiana na Musalia baada ya kugundua kuwa Ruto ambaye ni hasimu wao wa siasa alikuwa amealikwa kuwa mgeni wa heshima kwenye kongamano la wajumbe wa ANC, ishara ya mgawanyiko kwenye muungano huo. Akiwahutubia wajumbe kwenye kongamano hilo, Ruto ametangaza kuwa mikutano ya pamoja ya hadahara itaanzia Nakuru, siku ya Jumatano kabla ya kuandaliwa Magharibi na Kati ya Kenya.

"Nataka kuthibitisha kwa niaba ya UDA na wafuasi wangu, kuwa tutafanya kazi pamoja na ANC, Ford Kenya na vyama vingine vyote, kwenye safari hii ya kuleta umoja nchini Kenya,” alisema William Ruto.

Ushirikiano huo mpya unajenga jukwaa la washindani wawili wakuu katika uchaguzi mkuu

Wahlen in Kenia Präsidentschaftswahlen Stimmabgabe Polizeischutz vor Wahllokal
Wakenya wakishiriki uchaguzi wa mwaka 2007Picha: AP

Muda mfupi baada ya ndoa ya Kenya Moja kuvunjika Kalonzo na Gideon kwenye taarifa kwa vyombo vya habari wamesema huu ni wakati wa kusitisha ushirikano wao wakiutaja kuwa ni mchezo mchafu wa siasa. Imebainika kuwa Musalia, Ruto na Wetangu'la wamekuwa wakishauriana kwa majuma kadhaa kuhusu ushirikiano mpya. Ushirikiano huo mpya sasa unajenga jukwaa la washindani wawili wakuu kwenye uchaguzi wa Agosti Tisa.

Hata hivyo haijabainika ni nani atakayepeperusha bendera ya ushirikiano huo mpya dhidi ya Raila Odinga wa Azimio la Umoja. Akielezea sera zake kwa taifa, Musalia aliishambulia serikali ya Rais Kenyatta kwa kushindwa kuinua uchumi wa taifa, hivyo kuyafanya maisha ya mkenya wa kawaida kuwa magumu. Raila alitajwa kuwa mradi wa serikali uliobuniwa baada ya salamu za heri.

"Sasa narudia ili kuondoa shauku, msimamo wa ANC kuhusu hiki kichekesho kinachoitwa Azimio ni kuwa hatutashirikiana nacho. Azimio limejengwa kwa maslahi ya watu wachache,” alisema Musalia Mudavadi

Musalia ambaye alilaani siasa za usaliti dhidi ya Raila, anaonekana kuwasaliti wenzake wa OKA ambao Duru zinasema kuwa watajiunga na Azimio la Umoja linaoongozwa na Raila Odinga.

Musalia na Ruto ndio viongozi pekee wa siasa ambao wamekuwa wakifanya kampeni wakitangaza kuinua uchumi wa taifa. Kichekesho ni kuwa makamu wa rais ni sehemu ya utawala wa Jubilee, anaoushambulia kwa kushindwa kuboresha maisha ya Mkenya. 

Shisia Wasilwa, Dw, Nairobi