1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eti atajiuzulu au la ?

9 Mei 2016

Uvumi kuhusu uwezekano wa kujiuzulu mwenyekiti wa SPD, Sigmar Gabriel, jinsi karata zinavyochanganywa kufuatia uchaguzi wa majimbo wa Machi 13 iliyopita na kishindo cha CSU ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/1IkJ5
Mwenyekiti wa chama cha SPD,makamo kansela na waziri wa uchumi Sigmar GabrielPicha: Imago/CommonLens

Tuanzie na eti eti kuhusu uwezekano wa kuachia ngazi Sigmar Gabriel kama mwenyekiti wa chama shirika katika serikali kuu ya muungano mjini Berlin-SPD. Gazeti la Hannoversche Allgemeine" linaandika: "SPD wanabidi wanuse kule kunakotokota na baadhi ya wakati kunuka. Hivyo ndivyo alivyosema wakati mmoja Sigmar Gabriel katika mkutano mmoja mkuu wa chama chake na kushangiriwa. Alikusudia watu kuwa karibu zaidi na wananchi, kuyajua maisha ya wananchi wa kawaida yakoje. Lakini kinachotokota leo hii katika chama cha Social Democratic cha Ujerumani ni uvumi. Eti Sigmar Gabriel atajiuzulu? Eti kachoka? Eti hataki tena? Gerhard Schröder aliwahi wakati mmoja kuwaonya wana SPD dhidi ya kumchubua sana mwenyekiti wao. Aliongeza kusema:"Msimfyetulie mcheza kinanda, inaweza kutokea, msimpate mwengine." Na onyo hilo la Schröder lina uzito mpaka leo.

Sigmar Gabriel hafikirii kung'atuka

Maoni sawa na hayo yametolewa pia na mhariri wa gazeti la "Emder" anaehisi:"Suala la kujiuzulu Gabriel halizuki kwa sasa. Hata hivyo mawazo kama hayo si ya bure. SPD kwasasa wamesalia kuwa chama kisichokiuka kiunzi cha asili mia 20 ya kura. Na hilo si kosa la Gabriel peke yake. Lakini pia kiongozi huyo wa SPD haonyeshi dalili ya kuwa na mkakati wa kuibadilisha hali hiyo. Mjadala kama Sigmar Gabriel anafaa kuwa mgombea kiti cha kansela wa chama cha SPD tayari umehanikiza chamani.Tatizo la chama hicho; hawana badala. Kwamba spika wa bunge la Ulaya Martin Schulz atawagutuwa wapiga kura wakichague chama cha SPD-ni shida sana kuashiria.

Muungano wa rangi ya Kiwi,Kenya au rangi za Taa za Barabarani

Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linazungumzia jinsi karata zinavyochezwa baada ya uchaguzi wa majimbo wa Machi 13 iliyopita."Vyama ndugu vya CDU/CSU na walinzi wa mazingira die Grüne hawakutafutana lakini wamekutana.Tamko hilo la naibu mwenyekiti wa chama cha CDU Thomas Strobl kuhusu serikali inayokuja ya muungano mjini Stuttgart, ambayo tayari imeshakamilika tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, linazihusu pia serikali mbili nyengine za muungano, mijini Magdeburg na pengine mjini Mainz. Ni Mchangayiko wa rangi unaotokana na hali ya dharura iliyoibuka jumapili ya Marchi 13. Kiwi katika jimbo la Baden-Württemberg, muungano unaojulikana kama Kenya unaovileta pamoja vyama vya CDU,SPD na walinzi wa mazingira die Grüne katika jimbo la Sachsen Anhalt na muungano wa rangi Nyekundu,Manjano na Kijani (SPD-FDP na die Grüne) katika jimbo la Rheinland Palatinate-yote hiyo hakuna aliyekuwa akiitaka.Lakini haimaanishi haina tija.

Na hatimaeGazeti la "Rheinplaz" linaandika kuhusu kishindo cha chama cha CSU kutaka kusimamisha mgombea wake katika uchaguzi mkuu mwaka 2017. Mhariri anakumbusha kishindo kama hicho kilichotolewa mwaka 1976 na mwenyekiti wa wakati ule wa chama hicho kidogo cha kusini mwa Ujerumani CSU,Franz Josef Strauß kiligeuka mbio za sakafuni, anasema. Anahoji kishindo kama hicho hakitakuwa na maana isipokuwa kuwagharimu waapiga kura vyama vyote viwili CDU/CSU.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga