Hali mbaya ya usafiri
21 Januari 2015Boti na mikokoteni inayokokotwa na punda vilitumiwa kusafirisha karatasi za kura katika maeneo hayo yaliyokumbwa na mvua. Mamlaka ya uchaguzi nchini Zambia imesema mpango wa kutumia ndege kusafirisha masanduku ya kupiga kura na maafisa wa usimamizi wa zoezi hilo katika maeneo ya mbali hapo jana ulivurugwa na mvua kubwa iliyoambatana na radi.
Wapigakura katika vituo kadhaa kati ya jumla ya vituo karibu 6,000 vya kupiga kura walitarajiwa kutekeleza jukumu hilo leo hii, katika kinyang'anyiro hicho kilichotokana na kifo cha aliyekuwa rais wa taifa hilo Michael Sata, mwaka uliopita.
Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi nchini humo katika eneo moja kwa mfano, vifaa vya kupigia kura, kwanza vitasafirishwa kwa boti, baadae maafisa wa usimamizi watapaswa kutembea kwa miguu kwa masaa matatu kabla hawajatumia mikokoteni ya kukokotwa na punda kuelekea katika vituo vya kupiga kura.
Malalamiko ya upinzani
Kitendo cha kuchelewa kufikishwa vifaa vya kupiga kura katika baadhi ya maeneo nchini humo, kumezusha kilio kwa upande wa upinzani. Mgombea kutoka chama cha upinzani Hakainde Hichilema kutoka chama cha upinzani cha UPND alilalamikia kufanyika kwa udanganyifu katika kinyang'anyiro hicho.
Mkurugenzi wa uchaguzi Priscilla Issacs alisema hawana namna ya kudhibiti matokeo ya hali ya hewa. Na mkuu wa timu ya waangalizi wa eneo la kusini mwa Afrika, Waziri wa Mambo ya nchi za nje ya Afrika Maite Nkoana-Mashabane ameitaka tume hiyo ya uchaguzi kufanikisha uchaguzi tulivu pamoja na changamoto hiyo ya hali ya hewa.
Kiasi ya watu milioni 5.2 wanatajawa kuwa na uwezo wa kushiriki uchaguzi huu, lakini idadi hiyo inaweza isikiea kutokana na kadia ya mvua.
Matokeo ya awali yameanza kutolewa katika baadhi ya maeneo ya mijini lakini matokeo rasmi yatarajiwe kutolewa Ijumaa. Katika duru ya mwanzo ya kuhesabu kura katika majimbo 150, inaonesha Edgar Lungu anaongoza kwa matautu na Hichilema moja. Mmoja kati ya wapiga kura alikuwa na haya ya kusema.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu kabisa wa kampuni yenye kujishughulisha na biashara na uchumi-Premier Consult alisema inaonesha wazi kabisa kinyang'anyiro hicho kikali, kwa kuwa wagombea kujongeleana kwa karibu katika matokeo.
Kambi ya Hichilema ianonekana kupanda nguvu kutokana na msuguano wa ndani wa chama kingine kikubwa cha upinzani cha MMD, ambacho mgombea wake Nevers Mumba amekuwa na nafasi ndogo ya kuibuka mshindi katika uchaguzi huo.
Mgombea Lungu wa chama tawala, ameingia katika mchuano katika wakati mgumu baada ya kutokea mvutano wa ndani wa kuwania madaraka baada ya kifo cha rais Sata Oktoba mwaka jana. Kwa mujibu wa benki ya dunia pamoja na sera zenye kuonesha ukuwaji na uchumi imara kwa miaka michache iliyopita kiasi ya asilimia 60 ya idadi jumla ya Wazambia milioni 15 katika kiwango duni cha maisha.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga