1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani

3 Desemba 2015

Kila tarehe 3 Disemba, dunia inaadhimisha Siku ya Watu wenye Ulemavu. Kauli mbiu ya mwaka huu wa 2015, ni ''Ushirikishwaji katika masuala mbalimbali: upatikanaji na uwezeshwaji kwa watu wote wenye uwezo.''

https://p.dw.com/p/1HGGV
Watu wenye ulemavu
Watu wenye ulemavuPicha: DW/H. Hashimi

Katika ujumbe wake kwa watu wenye ulemavu duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amesema maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika katika mwamko wa kuridhiwa kwa malengo mpya ya maendeleo endelevu ya umoja huo, hadi ifikapo mwaka 2030. Amesema mwongozo huo wa kimataifa unawataka kutomuacha mtu yeyote nyuma.

Ban amesema ili kuijenga dunia endelevu kwa ajili ya wote, unahitajika ushiriki wa watu wenye uwezo wote. Amefafanua kwamba ajenda ya mwaka 2030 inajumuisha masuala mengi ya kuwajali watu wenye ulemavu, na ni lazima wafanye kazi kwa pamoja ili kuzibadilisha ahadi hizo kuwa katika vitendo.

Amesema kwa kushirikiana na watu wenye ulemavu, dunia itaweza kusonga mbele bila ya kumuacha mtu yeyote nyuma. Mwaka ujao 2016, mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu makaazi (UN HABITAT III), utajadili ajenda ya maendeleo mapya ya mijini ili kuijumuisha miji, kuifanya iweze kupatikana na kuwa endelevu. Ban amesema sauti za watu wenye ulemavu zitakuwa muhimu katika mchakato huo.

Kwa mwaka huu, siku hii inaadhimishwa na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa, wataalamu huru na mashirika ya kiraia mjini Geneva. Maadhimisho hayo yanahusisha mfululizo wa shughuli zinazohusisha kuzungumzia mafaniko na mchango wa watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na kuthibitisha dhamira yao ya kupatikana haki kwa watu wenye ulemavu.

Takwimu za ulemavu kutumika kwenye utafiti

Nalo shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa limedhamiria kuendelea kukuza utoaji wa takwimu za ulemavu na zitakapokuwa tayari, zitazitumia katika utafiti wake na kazi, ikiwa ni pamoja na lengo la 5 la maendeleo endelevu kuhusu usawa wa kijinsia na kuwezeshwa wanawake wote na wasichana.

Kwa upande wake shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa-UNICEF, linaanzisha kampeni ya kimataifa ya ''kumaliza ukatili dhidi ya watoto na vijana wenye ulemavu''. Kampeni hiyo ya kwenye mitandao, itazingatia maeneo matano kuanzia kwenye unyanyapaa na ubaguzi, unyanyasaji wakati wa dharura na takwimu kuhusu ghasia. Kampeni hiyo inazinduliwa Disemba 3 mwaka huu na itaanza kutekelezwa mwaka ujao wa 2016.

Watu wenye ulemavu
Watu wenye ulemavuPicha: DW/H. Hashimi

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu bilioni moja ya idadi ya watu duniani, wana aina fulani ya ulemavu, na wamekuwa wakikumbana na vikwazo vingi ikiwemo kujumuishwa kwenye nyanja muhimu katika jamii. Kutokana na hali hiyo, watu wenye ulemavu hawafurahii ujumuishwaji wao katika jamii kwa misingi ya kuwa sawa na wengine, ikiwemo usafiri, ajira na elimu pamoja na ushiriki wa kijamii na kisiasa.

Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani imekuwa ikiadhimishwa tangu mwaka 1992 ili kukuza uelewa na kuhamasisha msaada katika masuala muhimu yanayohusiana na kujumuishwa watu wenye ulemavu katika jamii na maendeleo.

Serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiraia, taasisi za elimu na sekta binafsi, siku zote zimekuwa zikihamasishwa kushirikiana na mashirika ya watu wenye ulemavu ili kuandaa matukio na shughuli za kuiadhimisha siku hii.

Nchini Tanzania, idara inayowashughulikia watu wenye ulemavu-DDA, sekretarieti ya baraza la taifa la Zanzibar la watu wanaoishi na ulemavu, wameandaa mjadala kwa wanafunzi kutoka shule za serikali na zile binafsi.

Nako nchini Nigeria, shirika la kimataifa la afya kwa ajili ya watu wanaokabiliwa na changamoto, linashirikiana na viongozi wa kijadi kwenye miji ya Karu na Jikwoyi kuiadhimisha siku hii. Mashirika ya serikali, vyombo vya habari, watu mashuhuri na kiasi ya watu 70 wanaoishi na aina mbalimbali ya ulemavu, wanahudhuria.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/UN Website
Mhariri:Yusuf Saumu