SIPRI: Marekani ndio kinara wa uuzaji silaha ulimwenguni
9 Machi 2020Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2015 hadi 2019, biashara ya uuzaji silaha ilishamiri kwa asilimia 5.5 kutoka kipindi cha mwaka 2010 hadi 2014. Kulingana na taasisi hiyo iliyo na makao yake makuu mjini Stockholm, Sweden, Marekani pekee iliuza silaha kwa asilimia 36 ya mauzo yote ulimwenguni, katika nchi 96. Saudia Arabia imesalia kuwa mwingizaji mkubwa wa silaha kwa asilimia 12.
Mwenendo wa jumla unaashiria kuwa kuna ongezeko la mauzo ya silaha duniani, amesema mtafiti mwandamizi wa SIPRI Pieter Wezemann, akiongeza kwamba "tunaona pia dhahiri kwamba Marekani inazidi kuwa muuzaji mkubwa zaidi wa silaha". Nusu ya mauzo ya silaha za Marekani yalielekea Mashariki ya Kati.
Urusi iko nafasi ya pili katika biashara ya uuzaji silaha ikiwa imeuza moja ya tano ya silaha zote ulimwenguni. Kwa kipindi chote hicho, Urusi iliuza silaha katika jumla ya nchi 47 na nusu ya mauzo yake yalielekezwa India, China na Algeria. Hata hivyo mauzo ya silaha ya Urusi yamepungua kwa asilimia 18 kulinganisha na kipindi cha nyuma.
"Si kwamba Urusi haijaribu kuuza silaha lakini ni wanunuzi zaidi ambao wamepata ugumu kuendelea na kiwango cha zamani cha ununuaji wa silaha, mfano mzuri ni nchi kama Venezuela", amesema Wezemann.
Ufaransa inakamata nafasi ya tatu kwenye viwango hivyo ikiwa imeorodhesha kiwango kikubwa cha mauzo tangu mwaka 1990 kutokana na mikataba mikubwa na nchi za Misri, Qatar na India, imesema taasisi hiyo. Ujerumani na Chinani miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwenye biashara hiyo, ikifanya mauzo yote kwenye nchi tano zilizo juu kuwa asilimia 76.
SIPRIinaamini kwamba Saudi Arabia itaendelea kuwa kinara wa kuingiza silaha "kwa miaka mingi inayokuja". Ukanda wa Mashariki ya Kati kwa ujumla una uingizwaji mkubwa wa silaha kwa asilimia 35. Ukiondoa Saudia, nchi za Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Iraq na Qatar ni miongoni mwa mataifa 10 ambayo yanaongoza kwa kuagiza silaha.
Baada ya miaka kadhaa ya kushuka kwa biashara ya silaha, Ulaya imeshuhudia ongezeko kidogo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Nchi kadhaa za Magharibi na ulaya ya kati ziliamua kununua kwa mfano mifumo mipya ya ndege ambayo "ilitengenezwa Marekani", wakati Urusi ilipoitwaa Crimea mwaka 2014.
Vyanzo: dpa/afp