1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SIPRI: Nchi zenye silaha za nyuklia zaendelea kuziimarisha

15 Juni 2020

Taasisi ya SIPRI imesema idadi ya vichwa vya nyuklia imepungua hadi 13,400 mwaka huu. Lakini nchi tisa zenye silaha za kinyuklia zinazidi kuziimarisha kuwa za kisasa zaidi.

https://p.dw.com/p/3dlXK
Berlin Protest gegen Auflösung des INF-Vertrages
Picha: Imago Images/epd/C. Ditsch

Kwenye ripoti yake iliyotolewa leo Jumatatu, taasisi hiyo ya kimataifa ya utafiti wa amani na pia inayofuatilia biashara ya silaha (SIPRI) imesema kuwa kiujumla idadi ya vichwa vya nyuklia ilipungua ulimwenguni kwa 465 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka wa 2019.

Takwimu hiyo ilijumuisha vichwa vya nyuklia ambavyo vimeshaunganishwa kwenye makombora, ambavyo vimehifadhiwa pamoja na vinavyopaswa kukongolewa au kuharibiwa.

Kupungua kwa idadi hiyo kumetokana na kukongolewa kwa vichwa vya nyuklia vya zamani vya Urusi na Marekani.

Kwa pamoja mataifa hayo mawili yanamiliki asilimia 90 ya silaha zote za kinyuklia ulimwenguni.

SIPRI imekadiria kuwa Marekani inavyo vichwa vya nyuklia 5,800 huku Urusi ikiwa na vichwa 6,275 vya nyuklia.

Uingereza, Ufaransa, China, India, Pakistan, Israel na Korea Kaskazini ni miongoni mwa nchi ambazo zimetajwa kumiliki silaha za nyuklia.

Idadi ya vichwa vya nyuklia katika nchi mbalimbali

Taasisi ya SIPRI imekadiria kuwa Uingereza ina vichwa vya nyuklia 215, Ufaransa inavyo 290, China 320, India 150, Pakistan 160 na Israel 90. Korea ya Kaskazini inaaminika kumiliki kati ya vichwa 30 hadi 40, lakini havikujumuishwa kwenye makadirio ya taasisi ya SIPRI kuhusu idadi jumla ya vichwa vya nyuklia ulimwenguni.

SIPRI imesema kuwa takriban vichwa vya nyuklia 1,800 vimewekwa katika hali ya kuwa tayari sana kwa matumizi.

Marekani na Urusi zinaongoza katika umiliki wa silaha ya nyuklia ulimwenguni: SIPRI
Marekani na Urusi zinaongoza katika umiliki wa silaha ya nyuklia ulimwenguni: SIPRIPicha: Wkipedia/U.S. Air Force

Wakati huo huo, mataifa yenye silaha za nyuklia yamekuwa yakiziimarisha silaha zao au kutengeneza mifumo mipya, ikiwa ni pamoja na mifumo ya kurusha makombora na ndege na pia vituo vya kutengeneza silaha za nyuklia.

Mtafiti wa taasisi ya SIPRI Shannon Kile ameliambia shirika la habari la DPA kuwa nchi zote tisa ambazo zina silaha za nyuklia, zinaonekana kuziweka silaha zao kwa matumizi ya baadaye.

Kitisho kwa ulimwengu

Kile amesema hali hiyo inaashiria kwamba silaha za nyuklia zinaendelea kuchukuliwa kama kinga, lakini pia kuna ishara kwamba zinapewa majukumu mapya au yaliyotanuliwa katika mipango ya kijeshi, haswa nchini Marekani na Urusi.

Kile ameongeza kuwa "Hali hiyo inaashiria kurudisha nyuma hatua zilizopigwa baada ya Vita Baridi za kuondoa silaha za nyuklia kwa njia taratibu, na ninafikiri kinachohofisha zaidi ni kuendelea kuziimarisha.”

Ripoti ya SIPRI ilijikita kwenye duru za waziwazi. Taasisi hiyo imesema kuwa ukosefu wa uwazi wa mataifa yenye silaha za nyuklia ni changamoto.

Marekani, Uingereza na Ufaransa zinatoa baadhi ya taarifa, lakini Urusi inabadilishana tu taarifa na Marekani chini ya makubaliano kati yao yajulikanayo kama New START yaani mwanzo mpya yaliyosainiwa mwaka 2010 ya kupunguza silaha za nyuklia.

Korea Kaskazini haitoi maelezo kuhusu uwezo wake wa silaha za nyuklia japo, hukiri kufany amajaribio ya makombora na nyuklia: SIPRI
Korea Kaskazini haitoi maelezo kuhusu uwezo wake wa silaha za nyuklia japo, hukiri kufany amajaribio ya makombora na nyuklia: SIPRIPicha: picture-alliance/AP/Korean Central News Agency

"Makubaliano ya New START ni mkakati muhimu wa kuhakikisha kuna uwazi” amesema Kile akiongeza kuwa kwa mfano, yamezipa Marekani na Urusi nafasi ya kufanya ukaguzi wa  kimaeneo.

Marekani yataka kuihusisha China katika mazungumzo ya nyuklia

Wajumbe wa Marekani na Urusi wanatarajiwa kukutana baadaye mwezi huu mjini Vienna kujadili hatima ya mkataba huo wa New START ambao unatarajiwa kumalizika Februari 2021.

Kile amesema Marekani inataka kuihusisha China katika mazungumzo ya baadaye kuhusu uangamizaji wa silaha za nyuklia, mnamo wakati kuna wasiwasi kuwa China inaongeza silaha zake nyuklia na kutengeneza silaha zaidi za kinyuklia kwa vikosi vyake vya ardhini, majini na angani.

SIPRI imesema India na Pakistan hutoa taarifa kuhusu baadhi ya majaribio ya makombora lakini hutoa maelezo kidogo kuhusu idadi ya silaha zao.

Lakini Korea Kaskazini, haitoi kabisa taarifa kuhusu uwezo wake wa silaha za nyuklia, japo imekiri kufanya majaribio ya makombora na nyuklia.

Israel pia haitoi maelezo yoyote kuhusu silaha zake za nyuklia.

Vyanzo: DPAE, AFPE