1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sirte , Libya. Kikao cha tano cha viongozi wa umoja wa Afrika kuanza leo.

4 Julai 2005
https://p.dw.com/p/CExV

Kikao cha tano cha viongozi wa mataifa wanachama wa umoja wa Afrika kinachoanza leo Jumatatu katika mji wa Sirte nchini Libya utaliangalia kwa kina suala la uwakilishi wa Afrika katika baraza la usalama la umoja wa mataifa pamoja na uhusiano wa Afrika na mataifa yaliyoko katika kundi la G8 yaliyo na utajiri mkubwa wa viwanda duniani.

Kwa mujibu wa msemaji wa umoja wa Afrika Adam Thiam , jumla ya viongozi 40 kutoka idadi ya mataifa 53 wanachama wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo.

Miongoni mwa viongozi ambao tayari wako mjini Sirte tangu jana jioni ni pamoja na rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo, Jose Eduardo dos Santos wa Angola, Mathieu Kerekou wa Benin , Abdelaziz Bouteflika wa Algeria, Francois Bozize wa jamhuri ya Afrika ya kati, Laurent Gbagbo wa Ivory Coast , na Ismail Omar Guelleh wa Djibout.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Bwana Kofi Annan , ambaye anatarajiwa kuhutubia mkutano huo , pia amewasili mjini Sirte jana Jumapili. Ulinzi umeimarishwa katika mji huo pamoja na katika barabara zinazoelekea katika mji huo.

Kamishna wa umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso nae anatarajiwa kuhutubia mkutano huo.

Viongozi hao wa umoja wa Afrika wanatarajiwa wakati wa mkutano huo wa siku mbili kuidhinisha azimio juu ya uwakilishi wa Afrika katika baraza la usalama la umoja wa mataifa lililotayarishwa na kabla ya mkutano huo wa viongozi na mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa hayo.