Siwezi kumpigia goti Erdogan-Schulz
16 Septemba 2017Mgombea wa Ukansela wa chama cha Social Democratic SPD nchini Ujerumani Martin Schulz amezungumza na DW leo(16.09.2017) na kujieleza msimamo wake kuhusiana na masuala kadha ikiwemo pia mvutano na Uturuki pamoja na suala la mkataba wa wakimbizi uliofikiwa na Umoja wa Ulaya na Uturuki.Akihojiwa mjini Freiburg na mhariri mkuu wa DW Ines Pohl pamoja na mtangazaji Jaafar AbdulKarim -Schulz amesema ikilazimika mkataba juu ya wakimbizi ufutiliwe mbali Schulz amesisitiza kwamba Ujerumani haipaswi hata mara moja kujiweka chini mbele ya Uturuki.
''Siko tayari kumpigia magoti bwana Erdogan.Mtu hapaswi kuridhia kushinikizwa''
Ikiwa ni siku nane zimebakia kabla ya uchaguzi nchini Ujerumani mgombea huyo wa SPD amemkosoa kwa maneno makali rais wa Uturuki Erdogan akisema hali ya haki za binadamu nchini Uturuki imezidi kuwa mbaya.
''Kwa mwandishi habari yoyote atakayekwenda katika nchi hiyo kuripoti kwa hivi sasa siwezi kumhakikishia kwamba hatoishia jela''
Kadhalika Schulz amesema kwa hali inayoendelea hivi sasa nchini Uturuki chini ya rais Recepp Tayyip Erdogan haoni sababu yoyote ya nchi hiyo kupewa fursa ya kujiunga na Umoja wa Ulaya na kwamba haina maana yoyote kuzungumza na rais huyo wa Uturuki kwa sasa.
Ana mipango gani juu ya haki ya wahamiaji barani Ulaya
Schulz anataka kuwa muwazi akifanikiwa kuwa Kansela hata atakapozungumza na nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zinakwepa kuwapokea wakimbizi akisema
''ushirikiano ni kitu cha msingi katika masuala ya kusimamia gharama lakini pia kugawana wakimbizi''
Pia ametowa mwito wa kuundwa sheria ya Uhamiaji itakayoweka kiwango maalum katika Umoja wa Ulaya lakini vile vile sheria hiyo isiguswe. Akijibu suali aliloulizwa ikiwa anaweza kushirikiana na nchi zinazoendeshwa na madikteta barani Afrika ili mradi afikie lengo la kuwazuia wakimbizi kuingia barani Ulaya. Schulz amesema inawezekana kushirikiana na nchi za kanda hiyo hata zile ambazo hazizingatii utawala wa kidemokrasia kukabiliana na wimbi la wakimbizi wanaokuja Ulaya,lakini pia akasisitiza suala hili linawezekana tu kwa ushirikiano na usimamizi wa taasisi za Kimataifa.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Sudi Mnette