1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Slaa aachiwa huru kwa dhamana

Florence Majani18 Agosti 2023

Mwanasiasa mkongwe na mwanadiplomasia nchini Tanzania, Dk Wilbroad Slaa ameachiwa kwa dhamana.

https://p.dw.com/p/4VJgt
Dk Wilbroad Slaa, akiwa nyumbani kwake mara baada ya kuachiwa Ijumaa Agosti 18, 2023. Kulia ni Mwanasiasa James Mbatia na kushoto ni Askofu Emmaus  Mwamakula.
Dk Wilbroad Slaa (aliyeketi katikati), akiwa nyumbani kwake mara baada ya kuachiwa Ijumaa Agosti 18, 2023. Kulia ni Mwanasiasa James Mbatia na kushoto ni Askofu Emmaus Mwamakula.Picha: Florence Majani/DW

Dr. Slaa alikamatwa akituhumiwa kwa makosa ya uhaini.

Taarifa za kuachiliwa kwa Dk. Slaa zimekuja ndani ya masaa 24 baada ya jopo la mawakili wanaomtetea yeye na wenzake watatu kufungua kesi ya dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mwendesha Mashtaka Mkuu, Mkuu wa Polisi Mkoa wa Mbeya na Mkuu wa Polisi Kituo Kikuu cha Mjini Mbeya kwa kuendelea kuwashikilia wateja wao kinyume na taratibu za kisheria.

Mmoja wa mawakili hao, Dickson Matata, ameiambia DW kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno akisema na hapa namnukuu:

 "Muda huu nimepigiwa simu na uongozi wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam wakinijulisha kuwa Dr. Willibrod Peter Slaa walimtoa Mbeya usiku na wako naye kituoni hapo, hivyo nifike kwa ajili ya kufanya utaratibu wa dhamana yake nipo hapo na tayari nimekamilisha masharti na ameshapata dhamana.” 

Dk Slaa na wenzake, ni miongoni mwa wanasiasa na wanaharakati wanaopinga mkataba wa uwekezaji kati ya bandari ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai.

Yeye na wenzake watatu, Wakili Boniface Mwabukusi, na mwanaharakati wa kisiasa, Mdude Nyagali, walikamatwa kwa nyakati tofauti kati ya Agosti 11 na 13, na kuwekwa rumande wakikabiliwa na makosa kadhaa, yakiwamo ya uhaini, kwa mujibu wa upande wa serikali.

Katibu mkuu huyo wa zamani wa chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, alikamatwa na polisi Jumapili ya Agosti 13, wakati akizungumza kwenye mjadala uliokuwa ukirushwa moja kwa moja kupitia mtandao wa Clubhouse.

Slaa alipelekwa kituo cha polisi cha Mbweni na baadaye kituo cha Oyesterbay na siku moja baadaye, wakili wake Dickson Matata alisema mwanadiplomasia huyo amehamishiwa Mbeya, akijumuishwa na wenzake Nyagali na Mwabukusi.

Siku chache baada ya kukamatwa kwao, watetezi wa haki za binaadamu Tanzania na mashirika ya kimataifa, likiwemo la Amnesty international, waliibuka na kukemea kukamatwa kwa wanaharakati hao na kuitaka serikali kuwaachia bila masharti.

Hata hivyo, serikali ilikuwa imesema kuwa kukamatwa kwao hakukuwa na uhusiano wowote na upinzani wao dhidi ya mkataba wa bandari, bali kushukiwa kutenda matendo ya uhalifu.

 Florence Majani, DW . Dar es Salaa