Somalia yajiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki
6 Machi 2024Bendera ya Somalia ilipandishwa rasmi kwenye Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, mjini Arusha, Tanzania mnamo siku ya Jumatatu.
Hatua hiyo inafuatia Somalia kuwasilisha hati yake ya kuridhia kujiunga na Jumuiya hiyo kongwe zaidi barani Afrika.
Waziri wa Biashara na Viwanda wa Somalia, Jibril Abdirashid Haji Abdi, ndiye aliwasilisha hati ya kuridhia taifa hilo kuwa mwanachama rasmi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hati hiyo iliyokabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Peter Mathuki. "Hatua hii itaiwezesha Somalia kuchangia katika utekelezaji wa mipano mbali mbali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kama vile Umoja wa Forodha, Soko la pamoja, Umoja wa Fedha na Shirikisho la kisiasa,” amesema Mathuki.
Mathuki amebainisha pia kuwa Somalia itanufaika na miradi ya miundombinu ya kikanda kama vile barabara, reli na nishati.
Mogadishu yanuwia kutumia fursa na kukuza utengamano wa kikanda
Somalia -- taifa la pembe ya Afrika -- inajivunia ukanda wa pwani mrefu zaidi barani Afrika, wenye urefu wa zaidi ya kilometa elfu tatu na kwamba eneo hilo linaweza kutumika kama rasilimali ya kukuza uchumi wa bluu na kuongeza biashara ya kikanda ndani ya Jumuiya.
Akizungumza katika hafla ya kujiunga rasmi kwa nchi yake, mkuu wa ujumbe wa Somalia, Waziri wa Biashara na Viwanda wa Somalia, Jibril Abdirashid Haji Abdi, amesema taifa lake lina shauku ya kuchangia kuikuza Jumuiya hiyo hasa kwa mambo ya mtangamano kwa kutumia eneo lake la kimkakati na rasilimali za Taifa kwa manufaa ka kanda nzima.
"Tunatambua umuhimu wa kuongeza thamani kwa Jumuiya, kuimarisha ushirikiano na jirani zetu na kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii na programu za miradi ya pamoja,” amesema Haji Abdi.
Maombi ya Somalia kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki, yaliwasilishwa na rais wa nchi hiyo, Hassan Sheikh Mahmoud, wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi wa jumuiya hiyo uliofanyika jijini Arusha, Julai 22 mwaka jana wa 2023.
Mwanachama mpya, hali ya usalama na shauku ya kuitanua jumuiya kongwe zaidi barani Afrika
Kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya ya Afrika Mashariki, nchi nyingine inaweza kujiunga na jumuiya hiyo, endapo itaungwa mkono na nchi wanachama.
Vilevile iwapo nchi inayoomba itakuwa imetimiza masharti ya uongozi bora, demokrasia, inaheshimu sheria na haki za binadamu na kwamba iwe inapakana na miongoni mwa nchi wanachama.
Somalia inakadiriwa kuwa na idadi ya watu wanaofikia milioni 17 na kujiunga kwake na jumuiya ya Afrika Mashariki kunaifanya jumuiya hiyo kuwa na jumla ya mataifa nane. Mataifa mengine wanachama ni Tanzania, Kenya na Uganda ambazo ndiyo waanzilishi wa jadi wa jumuiya hiyo.
Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zilijiunga baadaye.
Hali dhaifu ya usalama nchini Somalia ni miongoni masuala yanayoweza kuibua wasiwasi wakati taifa hilo linaanza safari rasmi ya uanachama ndani Jumuiya ya Afrika Mashariki.