SpaceX na NASA kurusha chombo kipya kuelekea anga za juu
27 Mei 2020Hii itakuwa mara ya kwanza kufanyika na wanaanga wa Shirika la Anga za Juu la Marekani, NASA, kutokea kwenye ardhi ya nchi hiyo ndani ya kipindi cha miaka tisa.
Mkuu wa NASA, Jim Bridenstine, ameiita hatua hii kuwa ni ndoto ya muda mrefu ya Marekani, yaani kurusha chombo cha Kimarekani, kutokea ardhi ya Marekani, kikiwa na wanaanga wa Kimarekani. Roketi kwa jina la SpaceX Falcon 9 lilitarajiwa kuanza safari kutoka Kituo cha Anga cha Kennedy majira ya saa 4:33 usiku kwa majira ya Marekani, kikiwabeba wanaanga Doug Hurley na Bon Behnken kwa safari ya masaa 19, wakiwa kwenye chombo chenye muundo mpya kiitwacho Crew Dragon kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga.
Kulisikika mshindo mkubwa kutoka eneo lile lile ambalo lilitumiwa na NASA kwenye safari ya mwisho ya angani, ambayo rubani wake alikuwa ni Hurley mnamo mwaka 2011. Rais Donald Trump na Makamu wa Rais Mike Pence walipangiwa kuweko kwenye eneo la Cape Canaveral kushuhudia safari hiyo kwa macho yao.
Hii ni mara ya kwanza kwa NASA kuruhusu kampuni binafsi kupeleka angani wanaanga wake. Lakini Doug Hurley, mmoja wa wanaanga hao amesema ushirikiano huu umempa hamasa kubwa. Hurley in mwanaanga mwenye uzoefu, na mara ya mwisho kabisa ndiye aliyekuwa kwenye safari ya angani na chombo kiitwacho Space Shuttle mnamo mwaka 2011.
Hata hivyo, mabadiliko ya sasa yako wazi hasa kwa namna bilionea Elon Musk alivyohakikisha kuwa chombo chake kinabeba kiwango cha juu cha ubunifu kama ilivyokuwa kwa magari aina ya Tesla ambako wahandisi wake huwa sio wanaoamuwa kipi kionekane vipi.
Safari ya leo kwenda angani inamaanisha kwamba sasa NASA haiko peke yake kwenye soko la masuala ya anga za juu, jambo ambalo anasema mkuu wa shirika hilo, Jim Bridenstine, kuwa ulikuwa uamuzi mgumu sana kuufikia.
Kwa utaratibu rasmi, safari kuelekea Kituo cha Kimataifa cha Anga ni ya majaribio. Inahusu kuonesha kwamba chombo hicho kinafanya kazi, kwamba mchakato uko sahihi, na kwamba mifumo inakwendana.
Kwa muda gani wanaanga hawa wawili watakaa kwenye kituo cha anga, bado hilo ni jambo lisilojulikana. Zinaweza kuwa wiki sita au miezi mitatu, hadi majaribio yote yakamilike, kwa mujibu wa NASA. Vile vile, wanaanga hawa wanaweza kukitumikia kituo hicho hadi wenzao watakapowasili kwa utaratibu wa kawaida mnamo mwezi Agosti.
NASA ilitoa tenda ya takribani dola bilioni nane kwa kampuni za Tesla inayomilikiwa na Musk, Mmarekani aliyezaliwa Afrika Kusini, na ile ya ndege ya Boeing, ili watengeneze mifumo kinzani ya kusafirisha wanaanga kupeleka angani. Boeing inatarajia kuzinduwa mfumo wake kwa jina CST-100 Starliner hapo mwakani.