SPD na mtihani mkubwa baada ya uchaguzi mkuu
27 Septemba 2013Wajerumani wameshapiga kura,lakini suala nani wataunda serikali bado halijajibiwa.Vyama vya Social Democratic SPD na walinzi wa mazingira die Grüne vinasita sita kujiunga na serikali ya muungano itakayoongozwa na Angela Merkel.Vinahofia visije vikakabwa kisiasa na natija zote kumuendeya kansela.Ndio maana wawakilishi zaidi ya 200 wa chama cha SPD wanakutana mjini Berlin kuzungumzia uwezekano wa kujiunga au la na serikali ya muungano pamoja na vyama ndugu vya kihafidhina vya Christian Democratic Union-CDU na Christian Social Union CSU.
Wanasocial Democratic wameondolewa patupu katika uchaguzi mkuu.Wamejikingia asili mia mbili na nusu tu za kura ziada ikilinganishwa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2009 na kwa namna hiyo hawajalifikia lengo walilokuwa wamejiwekea.Hata hivyo wanabidi washirikiane na vyama ndugu vya kihafidhina vilivyojipatia nguvu zaidi vya Christian Democratic Union-CDU na Christian Social Union-CSU.Hivyo ndivyo,wapigakura wengi wa Ujerumani-kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya umma,wanavyopendelea.Serikali ya mwisho ya muungano kama huo wa vyama vikuu kati ya mwaka 2005 hadi 2009,iliyoongozwa na kansela Angela Merkel inaangaliwa na wajerumani wengi kuwa ilifana.SPD lakini hawakufaidika na chochote.Katika uchaguzi mkuu mwaka 2009 walishindwa vibaya sana.Mpaka leo hawajafanikiwa kujitakasa na mkosi huo.
SPD hamkani
Hiyo ndio sababu kwanini miito ya kuundwa serikali ya muungano wa vyama vikuu inakisumbuwa vibaya sana chama hicho.Wanasocial Democratic wanahofia wasije wakakabwa na maguvu ya CDU/CSU na hatimae kutoweka.Wanahofia wasifikwe na yaliyokifika chama cha kiliberali cha FDP ambacho katika uchaguzi mkuu wa september 22 iliyopita,hawajafanikiwa hata kukiuka kiunzi cha asili mia tano kuweza kuwakilishwa bungeni mjini Berlin.Hofu kama hizo zimeenea pia katika shina la chama hicho cha SPD.Katika matawi ya chama hicho tangu majimboni mpaka katika miji sauti zinapazwa kutaka SPD ikalie viti vya upinzani bungeni.Wanahoji SPD ikishiriki katika serikali ya muungano pamoja na vyama ndugu vya CDU/CSU,haitaweza kutekeleza sera zake.
Wanachama wa SPD wanataka wapatiwe usemi
Hoja hizo zinatolewa pia na baadhi ya vigogo wa chama hicho mfano wa waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westfalia bibi Hannelore Kraft.
Ndio maana wakuu wa SPD wanakutana kwa kongamano maalum mjini Berlin kuzungumzia kama wajiunge au la na serikali ya muungano itakayoongozwa na kansela Angela Merkel.
Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel anahisi:"Bibi Merkel anabidi atamke Ujerumani anataka kuipeleka wapi,malengo yake ni yepi,yuko tayari kuafikiana kuhusu kitu gani.Na mie nnaamini hawezi kukwepa wajib huo."
Kama vyama ndugu vya kihafidhina CDU/CSU vitaridhia masharti yote yanayotolewa na SPD ,hakuna anaeamini .Hakuna pia anaeamini kama wanachama wa SPD wakiulizwa maoni yao kama chama chao kijiunge na serikali ya muungano wa vyama vikuu watakubali. Sauti zinapazwa kudai wanachama wa SPD waulizwe maoni yao kuhusiana na matokeo ya kongamano linalofanyika leo hii mjini Berlin.
Mwandishi:Marx Bettina(DW Berlin)/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Josephat Charo