1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Spika wa bunge la Sudan Kusini ajiuzulu

9 Desemba 2019

Spika wa bunge la Sudan Kusini amejiuzulu baada ya kushutumiwa na wabunge wenzake kwa kushindwa hadi wakati huu kuwasilisha ripoti jumla ya ukaguzi wa mahesabu ya serikali

https://p.dw.com/p/3USQc
Nationale gesetzgebende Versammlung des Südsudan
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/I. Billy

Spika wa bunge la Sudan Kusini amejiuzulu baada ya wabunge kutishia kumuondowa madarakani kwa kuzuia juhudi za kupambana na rushwa pamoja na usimamizi mbaya. Taarifa hizo zimetolewa leo na vyombo vya habari nchini humo.

Anthony Lino Makana anashutumiwa na wabunge wenzake kushindwa hadi wakati huu kuwasilisha ripoti jumla ya ukaguzi wa mahesabu ya serikali pamoja na ripoti ya kupambana na rushwa mbele ya bunge.

Aidha spika huyo anatuhumiwa kuwazuia wabunge kuwaita mawaziri kwa ajili ya kuhojiwa bungeni. Kwa mujibu wa hoja iliyowasilishwa na wabunge waliomtaka spika ajiuzulu, Makana pia anatuhumiwa kuidhinisha mkopo wa dola milioni 400 kutoka benki ya Afrexim bila ya kuuwasilisha bungeni kama inavyotakiwa kisheria.

Katika taarifa yake iliyotangazwa na shirioka la habari la Sudan Kusini spika amesema sababu iliyomfanya kujiuzulu ni kuonesha heshima kubwa kwa uongozi wa chama tawala cha SPLM kutokana na chama hicho kumuomba achukua hatua hiyo.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW