Spoti: FC Cologne yamtimua kocha Soldo
25 Oktoba 2010Mashabiki saba walikufa baada ya kukanyagwa na umati wa watu walikokuwa wanajaribu kuingia katika uwanja wa Nyayo kushuhudia mechi kati ya Gor Mahia na AFC Leopards.
Katika Bundesliga shoka lamuangukia kocha wa FC Cologne baada ya timu hii kuendelea kujipata pabayani na Claudio Pizzaro aipiku rekodi ya Giovane Elber ya raia wa kigeni kwa kutia magoli mengi katika Bundesliga.
Katika ligi ya Bundesliga hapa Ujerumani- masaibu ya FC Cologne yaliendelea mwishoni mwa juma na shoka likamuangukia kocha Mkroatia Zvonmir Soldo. Cologne ambao wanajivunia ushindi mmoja tu msimu huu, baada ya kucheza mechi tisa walinyamazishwa na Hanover kwa mabao 2-1 Jumapili. Kocha wa zamani wa Hamburg na Dortmund, Thomas Doll, ndie anayepigiwa upatu kujaribu kuzuia boti la FC Cologne lisizame zaidi.
Soldo anakuwa kocha wa pili kufungishwa virago katika Bundesliga msimu huu baada ya Christian Gross kuiaga Stuttgart. Na kama mambo ni haya, jee kocha wa Bayern, Louis van Gaal, aanze kutia kichwa maji kabla ya hajanyolewa? kwani mabingwa hao wa Ujerumani wanaonekana hoi msimu huu- na Ijumaa iliopita walisalia sare tasa na Hamburg katika kile Louis van Gaal alisema ni jambo la kuvunja moyo.
Hata hivyo mtaalam wa soka hapa Ramadhan Ali anasema anaamini Van Gaal atasalia uongozini, kwani huenda Ubabe wa Mainz na Dortmund ukawa kile wanasema .Mwenyekiti wa Bayern Munich Karl -Hanz Rummenige anasema bado wana imani na Van Gaal.Na tukiwa bado katika hapa Ujerumani, Mshambulizi wa Werder Bremen, Mperu Claudio Pizzaro ameipiku rekodi ya Giovane Elber, stadi wa zamani wa Bayern Munich na VFB Stuttgart, kwa kuwa raia wa kigeni kutia magoli mengi. Elber alitingiza wavu mara 133 aliposakata dimba hapa Ujerumani kati mwaka 1994 -2003.
Pizzaro ambaye alijiunga na Bremen 1999- alifunga bao lake la 134 katika ushindi wa pale Bremen wa mabao 4-1 dhidi ya Borussia Monchegdlabach.
Nchini Kenya mashabiki saba wa soka walikufa Jumamosi usiku baada ya kutokea msukumano wa kuingia katika uwanja wa Nyayo mjini Nairobi. Maelfu ya mashabiki walifika kushuhudia mechi kubwa baina ya mahasimu wawili wa jadi wa soka Kenya- Gor Mahia na AFC Leopards. Waziri Mkuu Raila Odinga ameagiza uchunguzi kuanzishwa mara moja na ripoti kuwa tayari katika wiki moja ijayo.
Katika Ligi ya Uingereza, Chelsea bado wako kileleni baada ya ushindi wao dhidi ya Wolverhampton, Ilhali Liverpool waliweka kando masaibu ya klabu na kuinyuka Blackburn Rovers mabao 2-1. Manchester City ambao wamesisimua msimu huu hawakuwa na jibu kwa vijana wa Arsenal Wenger waliposhindwa mabao 3-0. Chelsea wako kileleni kwa pointi 22, wakifuatiwa na Arsenal ilhali Manchester United waliweka kando sakata ya Rooney na kuchukua nnafasi ya tatu baada ya ushindi wao dhidi ya Stoke City jana. Mwandishi: Munira Muhammad/rtreMhariri: Othman Miraji.