Steinmeier avunja bunge kupisha uchaguzi wa mapema
27 Desemba 2024Baada ya rais Steinmeier kulivunja bunge la Ujerumani Bundestag, sasa nchi hiyo ina siku 60 kuandaa uchaguzi wa mapema unaotarajiwa kufanyika Februari 23. Katika hotuba yake kwa taifa Frank-Walter Steinmeier, amesema uthabiti wa kisiasa ni muhimu kwa taifa hilo.
"Nimeamua kulivunja bunge la 20 la Ujerumani na kuitisha uchaguzi mpya tarehe 23 Februari mwaka ujao. Katika nyakati ngumu kama hizi uthabiti unahitaji serikali inayoweza kuchukua hatua iliyo na wingi wa kutosha bungeni. Kwa hiyo ninaamini kwamba uchaguzi mpya sasa ndio njia sahihi kwa maendeleo ya nchi yetu," alisema Steinmeier.
Ujerumani yajiandaa kwa uchaguzi baada ya Scholz kupoteza kura ya imani
Uamuzi wa Steinmeier unatokana na ombi la kansela Olaf Scholz baada ya kushindwa kura ya imani Desemba 16 aliyoiitisha bungeni kuona iwapo wabunge bado wana imani na serikali yake. Viongozi wa bunge kutoka chama cha Scholz cha Social Democratic (SPD) na kambi ya upinzani ya wahafidhina ya CDU/CSU awali walikuwa wameshakubaliana juu ya tarehe hiyo ya uchaguzi.
Scholz aliitisha kura ya kuwa na imani baada ya kumfuta kazi Waziri wa fedha Christian Lindner wa chama cha Free Democrats FDP baada ya miezi kadhaa ya mvutano juu ya bajeti ya mwaka 2025. Baadae chama hicho kilijiondoa katika serikali ya muungano na kumuacha Scholz na serikali ya wachache ya vyama viwili vya Social Democrats, SPD, na kile cha Kijani au Die Grüne. Kushindwa kwa Scholz katika kura hiyo kulifungua uwanja wa kampeni kuelekea katika uchaguzi wa mwiezi Februari mwakani, huku mpinzani wake wa chama cha kihafidhina chake Friedrich Merz, akitarajiwa kushinda na kuchukua nafasi ya Scholz kama kansela mpya wa Ujerumani hii ikiwa ni kulingana na kura za maoni.
Je Scholz anawezakurejea tena madarakani?
Merz anadai kuwa serikali ya Scholz imeweka kanuni chungu nzima na kukwamisha ukuaji wa kiuchumi. Tayari wachambuzi wanasema huenda ikawa vigumu kwa Scholz kuchaguliwa tena kuwa kansela wa Ujerumani.
Kulingana na uchunguzi huo chama cha kihafidhina kimeonekana kuwa mbele ya chama cha SPD kwa pointi 10 huku chama cha siasa kali cha Alternative for Deutschland (AfD) kikiwa pia mbele kidogo kuliko chama cha Scholz cha SPD. Kiongozi wake Alice Weidel, huenda akashinda nafasi ya Ukansela, lakini vyama vingine vimesema havitajiunga na chama hicho kuunda serikali ya muungano hii ikimaanisha Weidel ana nafasi finyu ya kuchukua nafasi hiyo. Chama cha kijani nacho kimetabiriwa kuwa katika nafasi ya nne.
Scholz ahimiza kampuni kuwekeza zaidi nchini Ukraine
Masuala muhimu yanayolikumba taifa la Ujerumani kuelekea uchaguzi ni uhamiaji, kuimarisha uchumi na namna nzuri ya kuendelea kuiunga mkono Ukraine wakati ikipambana na uvamizi wa kijeshi kutoka kwa jirani yake Urusi na mzozo wa Mashariki ya kati. Steinmeier alitahadharisha kuwa chuki, vurugu na vitisho havipaswi kupewa nafasi katika kampeni za kuelekea uchaguzi.
(dpa, Reuters, AFP).