Steinmeier: Ulaya isaidie zaidi dhidi Ebola
20 Oktoba 2014Hayo Steinmeier ameyasema katika kongamano la Afya ambalo lilianza jana katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin. Akiuhutubia mkutano huo uliowajumuisha wataalamu wa tiba, waziri Steinmeier amesema Umoja wa Ulaya hauna budi kufanya juhudi za haraka na zenye ufanisi zaidi, katika kutumia uwezo wake kuunga mkono mapambano dhidi ya kuenea kwa maradhi hatari ya Ebola.
Amesema umoja huo unapaswa angalau kutuma ujumbe wake wa kiraiakatika nchi zilizoathirika zaidi magharibi mwa Afrika, akiongeza kuwa ujumbe huo utatoa fursa kwa nchi kupeleka madaktari. Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani amesema Ulaya haiwezi kuendelea kutazama kando.
''Hakuna tena mashaka yoyote kwamba leo kitisho cha afya chenye kuvuka mipaka ya nchi kinahitaji mkakati wa kimataifa kuweza kuondolewa. Tusipochukua hatua sasa, matokeo ya siku za usoni hayawezi kutabirika, hata kwa Ujerumani. Tumesikia kilio cha nchi zilizoathirika zikiomba msaada mnamo wiki hizi chache, hatupaswi kuzitelekeza nchi hizo, na hatutafanya hivyo.'' Amesema Steinmeier.
Mkakati wa dharura kwa siku zijazo
Steinmeier amesema ukubwa wa kitisho cha Ebola unapaswa kukabiliwa kwa kutumia uwezo wote zilio nao nchi za Ulaya katika sekta za kijeshi na mahusiano na nchi za nje, na kuushauri Umoja wa Ulaya kuweka mkakati wa dharura unaojumuisha madaktari na vifaa, kwa ajili ya kukabiliana haraka na vitisho vingine vitakavyojitokeza siku za usoni.
Huku hayo yakiarifiwa, mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana hii leo mjini Luxembourg kutafakari mpango wa pamoja wa kupeleka msaada magharibi mwa Afrika, wakati ikielezwa kuwa kitisho cha Ebola kimefika katika kiwango cha kutisha.
Muda wa maneno matupu umekwisha
Awali, rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf alikuwa ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, akitaka msaada zaidi kwa nchi yake pamoja na Guinea na Sierra Leone. Bi Sirleaf amesema kizazi kizima kinakabiliwa na hatari ya kuangamia, na kuonya kuwa muda wa ahadi na maneno matupu ulikuwa umekwisha.
Mwanadiplomasia mmoja amesema meli ya kijeshi ya Uingereza ambayo iko njiani kuelekea Sierra Leone ikisheheni vifaa na wafanyakazi, itaweka msingi wa kazi za Umoja wa Ulaya katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari.
Mwanadiplomasia mwingine amegusia mpango wa nchi tatu tajiri kuongoza juhudi za kimataifa katika nchi tatu zenye matatizo makubwa zaidi. Katika mpango huo Marekani itaisaidia Liberia, Uingereza itashughulikia Sierra Leone, huku Ufaransa ikielekeza juhudi zake kwa Guinea.
Huku Ebola ikizidi kusababisha hofu na maafa, habari njema kutoka Uhispania zimeeleza kuwa muuguzi aliyekuwa ameambukizwa Ebola wakiwatibu wamisionari wawili waliorudi nyumbani na ugonjwa huo kutoka Afrika Magharibi, amepona. Pia Nigeria inatarajiwa kutangazwa kama nchi ambayo haina tena maambukizi ya Ebola, miezi mitatu tu baada ya visa kadhaa vya ugonjwa huo ambavyo vilizusha hofu ya mripuko katika nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.
Tangu kutokea kwa mripuko mpya wa Ebola magharibi mwa Afrika, watu wapatao 9,200 wamambukizwa, na 4,555 kati yao tayari wamekufa, hii ikwa ni kwa mujibu wa takwimu mpya za shirika la afya ulimwenguni, WHO.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman